Na John Bukuku – Sinza, Kinondoni Kusini
Msako mkali dhidi ya wizi wa umeme unaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya Kinondoni Kusini ukiongozwa na Maafisa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakishirikiana na wakaguzi wa mita kwa lengo la kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria watumiaji wa umeme wanaokiuka taratibu
Timu ya mafundi wa umeme ikiongozwa na Afisa Uhusiano wa Wateja wa TANESCO ilifika katika Mtaa wa Alinuru eneo la Sinza kwa ajili ya kuhakiki mita za umeme nyumba kwa nyumba
Katika uhakiki huo ilibainika kuwa kuna sehemu tatu za biashara ambazo mita zake zilisoma maeneo tofauti na zilipo sasa jambo linaloashiria uwezekano wa uvunjaji wa sheria
Uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa Eneo la kwanza mita yake inasoma Kinondoni North, Eneo la pili mita yake inasoma Manzese Kilimani, Eneo la tatu mita yake inasoma Ubungo Mawasiliano
Hata hivyo mahojiano na wamiliki wa nyumba hizo hayakufanyika kwa sababu hawakuwepo ila wawakilishi wao walipewa barua za wito kufika ofisini kesho kwa maelezo zaidi Wawakilishi hao ni Mr. Amadi Mfundo Tito Emanuel na Rogers Muba
Timu ya TANESCO Kinondoni Kusini imetoa wito kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya wizi wa umeme na uhamishaji wa mita kutoka eneo moja kwenda jingine bila idhini au kibali cha shirika hilo
Aidha TANESCO imesisitiza kuwa watakaobainika wakichezea au kuharibu miundombinu ya umeme watakabiliwa na hatua kali za kisheria bila msamaha
Zoezi la msako na uhakiki wa mita ni endelevu na linatarajiwa kufanyika nchi nzima