Rais wa Kenya, William Ruto, leo amekutana na kikosi cha Harambee Stars na kutoa ahadi nono kuelekea mechi ya mwisho ya Kundi A ya michuano ya CHAN 2024 dhidi ya Zambia, itakayopigwa Jumapili katika Uwanja wa Kasarani.
Ruto amethibitisha kutimiza ahadi yake ya awali ya kuwapa wachezaji KSh milioni 1 (TSH 19.2 milioni) kila mmoja kwa kila ushindi wa mechi za makundi, lakini safari hii ameongeza dau, akiahidi KSh milioni 2.5 (TSh 48 milioni) kwa kila mchezaji endapo wataibuka na ushindi dhidi ya Zambia.
Zaidi ya hapo, Rais Ruto ameahidi kutoa KSh milioni 1 (TSH 19.2 milioni) na nyumba ya bei nafuu kwa kila mchezaji iwapo Harambee Stars watashinda mchezo wa robo fainali ya CHAN 2024.
Ahadi hizo zimechochea ari ya wachezaji na mashabiki, huku matumaini yakiwa juu kwamba timu hiyo itaandika historia mpya kwenye mashindano hayo.