MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata shehena ya dawa mpya ya kulevya aina ya mitragyna speciosa mifuko 756 yenye uzito wa jumla ya kilogramu 18,485.6 sawa na tani 18.5 iliyokuwa ikiingizwa nchini kama mbolea.
Hayo yamesemwa leo Agosti 13,2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa, katika tukio hilo watuhumiwa saba (7) wamekamatwa, wakiwemo raia wawili wa nchi ya Sri – Lanka ambao ni Jagath Prasanna Madduma Wellalage (46) na Santhush Ruminda Hewage (25).
Aliendelea kuwa, watanzania waliokamatwa ni Riziki Abdallah Shawej (40), Andrew Athanas Nyembe (34), Mariam Shaban Mgatila (40), Ramadhan Sanze Said (57) na Godwin Melchory Maffikiri (40).
“Dawa hizi zilikuwa kwenye kontena lenye ukubwa wa futi 40, zikitokea nchini Sri – lanka. Hii ni mara ya pili kukamatwa kwa aina hii ya dawa mpya ya kulevya, ambapo mwezi Juni mwaka huu, tulikamata mifuko 450 yenye zaidi ya uzito wa tani 11.5 za dawa hiyo mpya ya kulevya aina ya mitragyna speciosa iliyoingizwa nchini kama mbolea ikiwa kwenye kontena lenye ukubwa wa futi 20 ikitokea nchini Sri – Lanka ikiwahusisha watajwa hapo juu. Hivyo, kufanya jumla ya kilogramu 30,082.03 sawa na tani 30 za dawa hizo kukamatwa kwa kipindi kifupi hapa nchini.”
Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa, Mitragyna Speciosa ni dawa mpya ya kulevya (New psychtropic Substance-NPS) inayotokana na mmea unaofahamika kwa jina la Kratom ambao hupatikana zaidi katika nchi za Kusini Mashariki mwa Bara la Asia.
Amesema,dawa hiyo ya kulevya ina madhara sawa na dawa za kulevya jamii ya Afyuni (Heroin, Morphine).
“Dawa hii huathiri mfumo wa fahamu pamoja na kusababisha uraibu na vifo vya ghafla. Kutokana na kuongezeka matumizi ya dawa ya Mitragym Speciosa duniani, pamoja na madhara yanayosababishwa na sumu zilizomo katika dawa hii, nchi nyingi duniani zimezuia uzalishaji, usafirishaji na matumizi yake.”
Vilevile, Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa, ukamataji wa Mitragyna Speciosa ni ishara ya kuwepo kwa changamoto mpya katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini. Hivyo tutaendelea kuimarisha ufuatiliaji na udhibiti zaidi wa biashara ya dawa hii pamoja na dawa nyingine za kulevya hapa nchini.
Kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050, jamii yenye afya ni ile ambayo watu wanapata ustawi wa kimwili, kiakili na kijamii ili kujenga taifa la watu wenye uwezo watu wenye uwezo ni nguzo muhimu ya kufikia malengo ya Dira 2050.
Kwa muktadha huo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, matumizi na biashara ya dawa za kulevya yana madhara yakiwemo ya kiafya, kijamii na jiuchumi.
“Hivyo,vita dhidi ya dawa za kulevya kutabadilisha mtindo wa maisha unaozingatia misingi iliyowekwa na kufikia malengo ya Dira ya Taifa mwaka 2050 kwa ufanisi mkubwa kwa kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini na kulinda nguvu kazi ya Taifa. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, inaendelea na kasi ya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kuendelea kuvunja mitandao ya dawa za kulevya na kubaini mbinu mpya za biashara na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo kuongeza wigo wa utoaji elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya kwa lengo la kujenga jamii imara na kulinda ustawi wa jamii kwa maendeleo endelevu,”amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.