BOURNEMOUTH: KLABU ya Bournemouth imekamilisha usajili wa beki wa kati raia wa Ufaransa Bafode Diakite kutoka Lille kwa mkataba wa miaka mitano na kumfanya beki huyo kuwa usajili wa pili wa gharama kubwa zaidi katika historia ya kilabu hiyo.
Vyombo vya habari vya England vimeripoti ada ya usajili wa beki huyo kuwa ni euro milioni 35 pamoja na euro milioni 5 kama nyongeza likiwa dau la pili ghali zaidi nyuma ya pauni milioni 40.2 Bournemouth iliyolipia kumnasa Evanilson mwaka mmoja uliopita.
Diakite anaungana moja kwa moja na kikosi cha Andoni Iraola ambaye anakabiliwa na kibarua Kizito mbele ya mabingwa watetezi Liverpool katika mchezo wa kwanza wa msimu mpya wa Ligi Kuu Ijumaa jioni uwanjani Anfield.
Kijana huyo wa miaka 24 alifunga mabao 13 katika mechi 112 akiwa Lille. Msimu uliopita Diakite alicheza michezo 48 akiingia kambani mara nne.
Ujio wake utaisaidia Bournemouth kuziba pengo kwenye eneo la ulinzi lilioachwa na beki Dean Huijsen aliyetimkia Real Madrid na Illia Zabarnyi aliyesaini na mabingwa wa ulaya Paris Saint-Germain.
“Ninajua kocha ana mawazo mazuri ambayo yanatuwezesha kucheza vizuri kwenye Ligi Kuu. Sasa niko hapa ni nafasi nzuri kwangu kuonesha jinsi ninavyoweza kusaidia timu hii kusonga mbele.”
“Mimi ni beki ambaye anapenda kuwa na mpira na kucheza nao na natumai kuonesha kipaji change nikiwa na mpira au bila mpira. Nitatoa kila nilichonacho kwa ajili ya timu na natumai nitakuwa na wakati mzuri hapa Pamoja.” – alisema Diakite katika taarifa ya kumtambulisha
The post Diakite aweka rekodi akitua Bournemouth first appeared on SpotiLEO.