DAR ES SALAAM:KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Morocco amesema kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinaweka rekodi ya kumaliza hatua ya makundi ya michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) kwa kuhakikisha wanashinda michezo yote.
Stars iliyovuna pointi tisa katika michezo mitatu imebakisha mchezo mmoja dhidi ya Central Afrika utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Akizungumza kwenye mazoezi ya kikosi hicho, Morocco amesema licha ya kuwa kundi ni gumu, wachezaji wameonesha kujituma na kufuata maelekezo, jambo lililowapa matokeo chanya.
“Nishukuru wachezaji kwa kupambana, tunastahili pointi tulizopata. Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa sapoti yake, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na mashabiki kwa kutupa moyo na nguvu. Naamini tutafanya vizuri kwenye mechi zijazo,” amesema Morocco.
Kwa upande wake, Ofisa Habari TFF, Clifford Ndimbo, amesema maandalizi yanaendelea kwa mchezo wa Jumamosi dhidi ya Central Afrika, ukiwa ni wa mwisho wa hatua ya makundi.
“Tunataka tumalize vinara tukiwa na pointi 12 ili tupate nafasi ya kucheza Uwanja wa Benjamin Mkapa. Tukikosa nafasi hiyo, tunaweza kucheza uwanja mwingine. Kiingilio ni Sh 2,000 kwa mzunguko. Ni wakati mwingine tena watanzania kuungana kuisapoti timu yetu,” amesema Ndimbo.
Beki wa Taifa Stars, Dickson Job, amesema mechi hiyo ni muhimu kwa kujenga kujiamini kuelekea robo fainali.
“Tunahitaji kushinda ili kujiamini kwa mechi zijazo. Kila mchezaji ana nafasi ya kuandika historia katika maisha yake,” amesema Job.
The post Taifa Stars yataka rekodi Jumamosi first appeared on SpotiLEO.