Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Vijana wapatao 265,000 nchini wanatarajiwa kunufaika na fursa za ajira na kipato kupitia bunifu za kidigitali katika sekta ya kilimo, kupitia mradi wa Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture (YEFFA) unaofadhiliwa na Shirika la AGRA Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Sahara Accelerator.
Akizungumza katika kikao na vijana jijini Dar es Salaam, Adam Mbyallu kutoka Sahara Accelerator alisema mradi huo umeandaa ufadhili wa dola milioni 20 kusaidia ubunifu wa kilimo kwenye mnyororo wa thamani wa mazao manne—mbogamboga na matunda, alizeti, mpunga na mahindi.
“Tunalenga kusaidia vijana wenye bunifu zinazojibu changamoto za upatikanaji wa vifaa vya kilimo kupitia teknolojia za kidigitali, pamoja na kuwapatia mafunzo, mentorship na kuwaunganisha na wadau muhimu ili waweze kuzifikisha bunifu zao sokoni,” alisema Mbyallu.
Alibainisha kuwa bunifu zitakazochaguliwa zitalenga kutatua changamoto mbalimbali katika kilimo kama uhaba wa vifaa na mafundi, masoko, udhibiti wa mazao, na uharibifu wa mazao baada ya mavuno.
Kwa mujibu wa Mbyallu, dirisha la usajili wa bunifu limefunguliwa kwa muda wa miezi miwili na litafungwa Agosti 18, 2025, ambapo bunifu zitakazokidhi vigezo zitaunganishwa na wadau wa sekta ya kilimo wakiwemo wauzaji na watengenezaji wa zana, mafundi, taasisi za kifedha na mashirika mengine yanayohusiana.
Bunifu hizo pia zitagawanywa kwa kuzingatia kanda na aina ya zao; Morogoro itajikita kwenye mbogamboga na alizeti, Mbeya kwenye mbogamboga na mpunga, Njombe kwenye mbogamboga na mahindi, huku Singida ikilenga alizeti.
Mradi huu unatarajiwa kuongeza ajira kwa vijana, kuongeza tija kwenye kilimo na kuchochea matumizi ya teknolojia katika sekta hiyo muhimu ya uchumi.