DAR ES SALAAM: WALIMU wa mchezo wa ngumi 36 kutoka mataifa ya Tanzania (30), Ethiopia (3), Malawi (1), Comoros (1) na Bangladesh (1) wamemaliza mafunzo ya Kimataifa ya Ualimu ya Nyota moja yaliyofanyika Dar es Salaam.
Mafunzo hayo na Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), yaliendeshwa na Mkufunzi Mkuu wa Chama Cha Ngumi cha Dunia na Chama Ngumi cha Ulaya Dr. Gabriel Martelli kwa njia ya mtandao na darasa maalumu katika jengo la CCM kata ya Manzese, Dar es salaam.
“Ni hatua kubwa na yakujivunia katika mipango yetu BFT kuleta maendeleo na mapinduzi katika mchezo wa ngumi hasa kwa kuwezesha mafunzo ya Kimataifa kwa walimu wetu nchini,
“Tutaandaa mafunzo mengi zaidi ili kuongeza wigo kwa wanufaika. Tunamshukuru Mungu kwa kila hatua, tunaendelea kutekeleza kwa vitendo” alisema Rais wa BFT Lukelo Willilo.
Walimu walionufaika katika mafunzo hayo wa hapa nchini walitokea katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Kagera na Mwanza pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama vya JWTZ, JKT, Polisi na Magereza.
Shirikisho hilo linatarajia kuendesha mafunzo mengine ya walimu ya kimataifa hapo baadaye mwaka huu nchini Tanzania kwa kulenga walimu 50 kuweza kunufaika
The post Walimu 36 wa ngumi Afrika wanolewa first appeared on SpotiLEO.