LIVERPOOL: KATIKA harakati za kijiimarisha kuelekea msimu mpya Meneja wa mabingwa watetezi wa ligi kuu ya England Liverpool Arne Slot amethibitisha kuwa klabu hiyo imekubali dili la kumsajili beki Giovanni Leoni mwenye umri wa miaka 18 kutoka Parma siku moja kabla ya mechi yao ya ufunguzi dhidi ya AFC Bournemouth.
Vyombo vya habari vya England vimeripoti kuwa ada ya uhamisho ya mchezaji huyo wa Serie A inafikia euro milioni 26 ambayo ni sawa na kitita kinono cha shilingi za Kitanzania Bilioni 76.03.
Leoni tayari yuko njiani Kwenda Anfield na anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu baadae leo hii kisha atajiunga mara moja na kikosi cha kwanza huku klabu hiyo ikiondoa uwezekano wowote wa kumchukua kwa mkopo.
Kinda huyo ataungana na wakali Virgil van Dijk, Ibrahima Konate na Joe Gomez ambaye ana hatihati ya kuwa sehemu ya mchezo huo wakati huu anapata nafuu kutokana na jeraha la Achilles
“Kuna sababu zake Kiwango hapa ni 10/10, tunafanya kila kitu vizuri lakini ‘vizuri’ haitoshi. Tunapaswa kupiga hatua mbele zaidi. Mechi ijayo ijumaa jioni dhidi ya Bournemouth, hakuna visingizio.” Slot amesema
Slot ameongeza kuwa wana uharaka wa usajili wa mchezaji huyo kwa sababu mbalimbali kama vile majeruhi, mchanganyiko na muunganiko wa wachezaji wapya ndani ya kikosi hicho.
Vijana wa Slot wanaanza kutetea taji lao mbele ya Bournemouth kesho Ijumaa katika usiku ambao utakuwa wenye hisia kali katika dimba la Anfield kufuatia kifo cha mshambuliaji wao Diogo Jota na mdogo wake katika ajali ya gari mwezi Julai.
The post Liverpool yamnasa Leoni jioooni first appeared on SpotiLEO.