UDINE: MABINGWA wa Ulaya Paris St Germain walionesha ukubwa wao baada ya kupambana kutoka kufungwa 2-0 na kusawazisha dakika tano kabla ya mchezo kutamatika na hatimaye kushinda 4-3 kwenye mikwaju ya penalti dhidi ya washindi wa Europa League Tottenham Hotspur katika mchuano mkali wa UEFA Super Cup usiku wa Jumatano.
Totteham walionekana kuwa na uchu wa kumpa meneja wao mpya Thomas Frank mwanzo wa ushindi kabla ya mchezaji wa akiba wa PSG, Lee Kang-in kurudisha bao dakika 85 na Goncalo Ramos kufunga kwa kichwa dakika za lala salama na kusawazisha na ubao wa matokeo kuwa 2-2.
PSG walikamilisha ‘shoo’ hiyo kwa mikwaju ya penalty ya Goncalo Ramos, Ousmane Dembélé, Kang-In Lee, na Nuno Mendes baada ya Vitinha kukosa mkwaju wa kwanza huku Mathys Tel na Micky van de Ven wakikosa kwa upande wa Tottenham.
Wachezaji wa PSG walimiminika uwanjani kushangilia wakijua watakumbukwa daima kwenye historia ya klabu hiyo kama kikosi cha kwanza cha timu hiyo pia kuwa timu ya kwanza ya Ufaransa kubeba kombe hilo.
“Inafurahisha kushinda kwa namna hii. Timu hii kwa mara nyingine imeonesha kaliba yake hata kama tunakubali kuwa hatuko katika ubora wetu na utimamu kimwili. Tulifanikiwa kupata mabao tuliyohitaji kupitia wachezaji wa akiba (sub) na katika mikwaju ya penalti tuna wachezaji wanaopiga penalti vizuri na golikipa aliyetusaidia kushinda.” beki wa PSG Marquinhos alisema.
Tottenham ambao walimaliza katika nafasi ya 17 kwenye Ligi Kuu msimu uliopita walichukua uongozi wa mchezo huo baada ya Van de Ven kufunga kwa mpira ‘rebound’ kisha Cristian Romero kutanua uongozi huo alipofunga goli la pili kwa kichwa dhidi ya mabingwa hao wa Ufaransa ambao walishinda Kombe lao la kwanza la UEFA mwezi Mei kwa ushindi mnono wa mabao 5-0 dhidi ya Inter Milan.
Kiungo mshambuliaji wa PSG Lee Kang-in alifunga kwa mkwaju mkali baada ya timu yake kutawala karibu kipindi chote cha pili kabla ya Goncalo Ramos kukutana na krosi ya Ousmane Dembele kwa kichwa na kupelekea mchezo kumalizwa kwa mikwaju ya penalty.
“Ni ngumu kuzungumzia mechi hii. Tumefanya mazoezi kwa siku tano au sita pekee ni jambo la kushangaza kwakweli Kwetu ilikuwa muhimu sana kushinda kombe hili na kuwapa mashabiki wetu” alisema Luis Enrique kocha wa PSG.
The post PSG yaanza ubabe Ulaya first appeared on SpotiLEO.