UDINE: MABINGWA wa Europa League Tottenham Hotspur wamelaani vikali na kuchukizwa na vitendo vya ubaguzi wa rangi mtandaoni unaomlenga mshambuliaji wao Raia wa Ufaransa Mathys Tel baada ya klabu hiyo kupoteza kwa penalti kwenye mchezo wa UEFA Super Cup dhidi ya Paris Saint-Germain usiku wa Jumatano.
Washindi hao wa Europa League walipoteza uongozi wa 2-0 kisha kukosa kombe mbele ya PSG kwa penalty 4-3 katika mechi ya Super Cup iliyochezwa mjini Udine, Italia huku beki huyo na mchezaji mwenzie Mholanzi Micky van de Ven wakikosa mikwaju ya penalti.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo imesema watashirikiana kikamilifu na mamlaka za uchunguzi ili kuhakikisha wahusika wanafikishwa kwenye vyombo vya sheria na kuhakikisha hatua kali za kisheria zinachukuliwa.
“Tumechukizwa na unyanyasaji wa kibaguzi wa rangi ambao mchezaji wetu Mathys Tel amepokea kwenye mitandao ya kijamii kufuatia kupoteza mchezo wetu wa jana usiku wa UEFA Super Cup”.
“Mathys alionesha ujasiri mkubwa wa kuchukua jukumu la kupiga mkwaju wa penalty, wanaomnyanyasa ni watu waoga na hawajui wanachofanya wanajificha nyuma ya majina ya watumiaji na ‘profiles’ ambazo hazijulikani na kutoa maoni yenye chuki”.
“Tutashirikiana na mamlaka na mitandao ya kijamii kuchukua hatua kali iwezekanavyo dhidi ya mtu yeyote ambaye tunaweza kumtambua kuwa alihusika na ubaguzi. Tunasimama nawe, Mathys.” – Spurs imesema katika taarifa hiyo
Tel mwenye umri wa miaka 20 alisajiliwa na Spurs kwa mkataba wa kudumu baada ya muda wa mkopo wa miezi minne katika klabu hiyo ya Premier League kutamatika akitokea Bayern Munich ya Ujerumani mwezi Juni.
The post Spurs yalaani vikali ubaguzi kwa Mathys Tel first appeared on SpotiLEO.