Ofisa Habari wa klabu ya Azam FC, Hasheem Ibwe, amesema moja ya uwekezaji mkubwa wa maana ilioufanya msimu huu ni kumpata, Florent Ibenge, ambaye wana matumaini naye kuwa safari hii atawapeleka kwenye hatua za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
Ibwe amesema hayo siku chache baada ya droo ya Kombe la Shirikisho, ambapo timu hiyo imepangwa kuanzia ugenini dhidi ya Al-Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini, Septemba 19, kabla ya kurudiana, Septemba 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Ofisa habari huyo alisema pamoja na ugumu wa mashindano hayo, lakini uwapo wa Ibenge, kocha ambaye amekuwa na mafanikio makubwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, kila timu anayokwenda, wana imani kubwa ya kufanya vema.
“Al-Merreikh Bentiu hatuifahamu sana, ingawa tunaambiwa baadhi ya watu wa benchi la ufundi ni Watanzania, lakini tunajua pia tukivuka hapo tutacheza na mshindi kati ya KMKM dhidi ya AS Port ya Djibouti.
“Hizi ni timu tatu ambazo zimestahili kuwapo hapo, lakini zina bahati mbaya kwa kukutana na Azam FC ambayo imeimarika zaidi msimu huu, inayonolewa na Ibenge, kocha ambaye ana historia nzuri sana kwenye michuano hii ya kimataifa, timu anazofundisha huwa haziishii karibu, tuna matumaini ya kufanya vema msimu huu kuliko wakati mwingine wowote,” alisema Ibwe.
Azam msimu huu itakuwa chini ya Ibenge, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ambaye amekuwa na rekodi nzuri anapozifundisha timu kiasi cha kuwa mmoja wa makocha mwenye gharama kubwa Afrika.
Ameshawahi kuzifundisha timu za AS Vita ya DR Congo, RS Berkane ambayo aliipa ubingwa na Kombe la Shirikisho, kabla ya kuhamia Al Hilal ya Sudan ambayo aliiongoza hadi hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutolewa na kigogo, Al Ahly ya Misri.
Ofisa Habari huyo alisema katika michuano hiyo pamoja na kwamba inaonekana timu wanazocheza nazo ni za kawaida, lakini hawatoidharau timu yoyote.
NIPASHE