DAR ES SALAAM: Klabu ya Yanga imeomba radhi mashabiki na wanachama wake huku ikitoa ufafanuzi kuhusu mchango wa Sh milioni 100 uliotolewa katika Harambee ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Agosti 12, 2025 kuwa ulitoka GSM Foundation.
Ufafanuzi huo unakuja baada ya kuibuka mjadala kwenye mitandao ya kijamii na miongoni mwa wanachama wakilaumu uongozi wa klabu hiyo kujiingiza kwenye siasa na wengine wakihoji fedha hizo zimetoka wapi.
Hata hivyo, Klabu hiyo imeweka wazi kuwa fedha hizo hazikutoka kwenye akaunti wala mapato ya klabu.
Kwa mujibu wa taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa leo Agosti 14, 2025, na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga Andre Mtine, fedha hizo zilitolewa na GSM Foundation taasisi inayomilikiwa na mfadhili na mdhamini wa Yanga Ghalib Said Mohammed na sio kupitia hela za wanachama au kutoka kwenye mfuko wa klabu, kupitia vyanzo mbalimbali vya mapato.
“Uongozi wa Yanga unapenda kuomba radhi kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa mpira wa miguu kwa usumbufu wowote uliojitokeza kupitia sintofahamu hii,”imesema.
Taarifa hiyo imesema GSM Foundation imekuwa ikishirikiana na klabu ya Yanga kwa kipindi cha miaka mitatu kutoa fedha na misaada kwa jamii na makundi mbalimbali ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
The post Yanga yaomba radhi, yatolea ufafanuzi fedha CCM first appeared on SpotiLEO.