Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeishutumu Klabu ya Yanga kwa kile kinachodaiwa kuwa mchango wa Shilingi milioni 100 kusaidia kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikiutaja kama kitendo cha kukiuka kanuni za michezo na kuwagawa wanachama wake.
Katika taarifa yake ya Agosti 15, 2025, CHADEMA kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi Brenda Rupia, imesema maelezo ya Yanga yaliyotolewa Agosti 14, 2025 kwamba fedha hizo zilitolewa na mdhamini wao GSM kupitia taasisi ya GSM Foundation, yanakinzana na kauli ya awali ya Rais wa klabu hiyo, Mhandisi Hersi Said, aliyenukuliwa akisema Yanga imechangia CCM milioni 100 na GSM bilioni 10.
Chadema kimesema historia ya Yanga kama klabu iliyoasisiwa wakati wa harakati za kudai uhuru inapaswa kuilazimisha kubaki huru kisiasa na kulinda mshikamano wa mashabiki wake wenye itikadi tofauti, badala ya kuunga mkono chama kimoja.
“Kitendo cha Yanga kutumia fedha za wanachama wake ambao wengine sio wanachama wala mashabiki wa CCM, kuzipeleka kukisaidia chama kimoja (CCM) ili kiendelee kubaki madarakani ni kuwadharau wanachama wake wanaoamini kwenye vyama vingine”, taarifa hiyo imesema.
Chama hicho kimeituhumu Yanga kutumia fedha za wanachama wake, akiwemo wasiounga mkono CCM, kwa manufaa ya chama hicho tawala, jambo linalodaiwa pia kukiuka Ibara za 4, 12 na 17 za kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) zinazokataza vilabu na mashirikisho kujihusisha na siasa.
CHADEMA imetoa wito kwa Yanga kurudisha fedha hizo kwenye mfuko wa klabu, kuomba radhi kwa umma au kutangaza wazi kuwa ni tawi la CCM. Pia imewataka viongozi wa klabu hiyo kujitathmini iwapo wanastahili kuendelea kuongoza taasisi inayopaswa kuwa ishara ya mshikamano wa kitaifa.