

Rais wa Klabu ya Yanga SC, Hersi Said, ameshindwa kupenya katika mchujo wa wagombea ubunge wa Jimbo la Kongwa, ikiwa ni mara ya pili kwa mwaka huu jina lake kukatwa katika mchakato wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la Mwananchi, Hersi ameungana na wagombea wengine 11 waliokatwa, huku Isaya Mngurumi, aliyeshika nafasi ya pili kwenye kura za maoni za Agosti 4, 2025, akipata nafasi ya kuendelea.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala, alithibitisha kuwa Hersi alikuwa miongoni mwa makada 24 waliokuwa wakiwania ubunge wa jimbo hilo. “Ni kweli Hersi ni miongoni mwa wapenzi wa nafasi ya ubunge ndani ya chama chetu. Subirini, taratibu zingine tutawajulisha, bado tunasubiri majina tuanze kampeni,” alisema Mkaugala.
Hata hivyo, jina la Hersi halikujumuishwa katika orodha ya wagombea waliopitishwa, sambamba na Mwalimu Deus Seif, aliyeshika nafasi ya tatu kwenye kura za maoni.
Hii ni mara ya pili Hersi kukatwa mwaka huu, baada ya kushindwa kuingia kwenye mchujo wa Jimbo la Kigamboni ambapo jina lake halikujumuishwa katika orodha ya walioteuliwa.