Na.Sophia Kingimali.
Waandishi wa habari Nchini wanetakiwa kuzingatia Maadili na Misingi ya kazi hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuepuka habari za kichochezi zitakazopelekea kuvunja amani ya nchi badala yake wanapaswa kutenda haki kwa kuandika habari kwa kufuata sheria lakini pia kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa.
Wito huo umetolewa Jijini Dar es salaam na Mwakilishi Mkazi wa Taasisi ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS) Peter Koch wakati akifungua mafunzo ya siku moja kwa Waandishi wa habari nchini ambayo yameratibiwa kwa ushiriakiano wa Madia Brains pamoja na KAS lengo likiwa kuwajengea uelewa waandishi kuhusu sheria mpya ya uchaguzi wa Rais,Wabunge na madiwani ya mwaka 2024 pamoja na sheria ya tume huru ya uchuguzi.
Koch, amesema vyombo vya habari ni nguzo muhimu katika kulinda Demokrasia,vikihusisha wananchi na viongozi,hivyo waandishi wanapaswa kuepuka upendeleo,kutoa habari sahihi,kuheshimu faragha na kuepuka lugha ya chuki.
Aidha amesisitiza umuhimu wa mafunzo ya namna bora ya kuripoti habari zinazokuza uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika uchaguzi nyakati za uchaguzi.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Media Brains,Jesse Kwayu,amesema Waandishi wa habari wanapaswa kutumia kalamu zao kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi na kuchagua viongozi bora.
“Huu ni wakati wenu kama waandishi kuhakikisha mnawapa elimu wananchi ili waweze kufanya maamuzi sahihi ya kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano mkiwapa elimu watashiriki vizuri uchaguzi na kuwapa viongozi watakaofaa kwa maendeleo ya Taifa”,Amesema Kwayu.
Aidha meongeza kuwa Demokrasia hudhoofika pale uandishi unapokuwa wa uchochezi au wa upande mmoja, na kusisitiza kutoa nafasi sawa kwa wagombea wanawake na wanaume.
Nae Mkurugenzi Mwenza wa Media Brains, Absalom Kibanda, amewataka waandishi kufuata Maadili, miiko na sheria za uchaguzi wakati wautekelezaji wa majukumu yao.
Aidha amewataka pia kuepuka ushabiki wa kisiasa, na kuzingatia usalama wao wanaporipoti masuala ya kisiasa ili kuepuka kuligawa Taifa lakini pia kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi mkuu.