
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeitaka Klabu ya Yanga kujiepusha na Siasa huku kikieleza wasiwasi wake juu ya taarifa ya klabu hiyo ya Agosti 14, 2025, iliyodai mchango wa Shilingi milioni 100 iliyotoa kusaidia kampeni za uchaguzi za Chama cha Mapinduzi CCM ulitoka kwa GSM Foundation.
Taarifa ya leo Agosti 15, 2025 iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, CHADEMA imesema kitendo cha Yanga kuhusishwa na mchango huo ni kuingiza michezo kwenye siasa, jambo linalokiuka kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) zinazokataza vilabu kujihusisha na siasa
Taarifa hiyo imesema hatua hiyo inakinzana na misingi ya uhuru wa vilabu vya michezo na inakiuka Kanuni za FIFA (lbara 4, 12 na 17) zinazopiga marufuku vilabu kujihusisha na siasa huku ikisisitiza kuwa, Yanga kama klabu yenye wafuasi wenye itikadi mbalimbali za kisiasa, inapaswa kubaki huru, ikiunga mkono umoja na mshikamano wa wanachama wake, badala ya kuunga mkono chama kimoja.
CHADEMA imesema kitendo cha Yanga kutumia fedha za wanachama wake ambao wengine sio wanachama wala mashabiki wa CCM na kuzipeleka kuisaidia CCM ili iendelee kubaki madarakani ni kuwadharau wanachama wake wanaoamini kwenye vyama vingine na ni kinyume na historia ya vilabu vinavyounganisha Watanzania wote kupitia michezo.
Aidha CHADEMA imeitaka Yanga irudishe fedha hizo kwenye mfuko wa klabu au kutamka wazi kama klabu ni tawi la CCM, na pia iombe radhi kwa umma huku ikitoa wito kwa viongozi wa Yanga kujitathmini na kuzingatia uhalali wao wa kuongoza taasisi inayowaunganisha Watanzania wote bila kujali itikadi zao za siasa.