Klabu ya Young Africans SC imekanusha taarifa zilizoenea kuwa Rais wake, Injinia Hersi Said, alichukua fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kongwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Msemaji wa klabu hiyo, Ally Kamwe, akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigali, Rwanda Ijumaa hii, amesisitiza kuwa Hersi hakuchukua fomu katika jimbo hilo wala kuonesha dhamira ya kugombea nafasi hiyo.
“Injinia hajachukua fomu huko kunakotajwa. Shughuli zake na masuala ya kwenda bungeni yaliishia Kigamboni. Hajaonesha dhamira ya kuchukua fomu kwenye jimbo jingine lolote ndani ya Tanzania,” alisema Kamwe.
Msemaji huyo amefafanua kuwa mchakato wa kuchukua fomu unahitaji hatua kadhaa—ikiwemo kuchukua, kurudisha na kufanya kampeni—jambo ambalo Hersi asingeliweza kulitekeleza kutokana na kuwa na Yanga kwenye ziara ya michezo nchini Rwanda.
Kamwe amedai kuwa taarifa hizo ni sehemu ya njama za kujaribu kuvuruga mshikamano wa klabu.
“Hizi ni agenda za kuwaleta maadui ndani ya klabu yetu. Ndiyo maana unasikia mara Injinia amegombea huku, mara kule… Yote haya ni malengo maovu ya kuharibu amani, mshikamano na umoja wa klabu yetu,” aliongeza.
Awali, vyombo mbalimbali vya habari nchini, viliripoti kwamba jina la Hersi lilikuwa miongoni mwa majina 24 ya makada waliojitokeza kuwania ubunge wa Jimbo la Kongwa, lakini halikupenya katika mchujo wa awali.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, hii inakuwa mara ya pili jina lake kuondolewa kwenye mchakato wa ndani ya CCM, baada ya awali kushindwa kwenye Jimbo la Kigamboni.
Ingawa kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi ambalo Ijumaa hii liliripoti kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala alithibitisha jina la Hersi kuwa miongoni mwa makada waliojitokeza kugombea ubunge wa jimbo hilo, Yanga imeweka wazi kuwa Rais wake hajajihusisha na mchakato huo na kwamba taarifa hizo hazina ukweli wowote.
Mchakato wa uchukuaji fomu katika jimbo la Kongwa, Dodoma ulifanyika kufuatia kifo cha Spika wa zamani wa Bunge la Tanzania, Mhe.Job Ndugai, aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo na ambaye alifariki dunia August 6, 2025