DAR ES SALAAM: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa katika sekta ya michezo chini ya Serikali ya Awamu ya Sita umeifanya Tanzania kuwa kitovu cha michezo barani Afrika.
Msigwa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifugua Mkutano wa Pili wa Baraza la Mawaziri wa Michezo wa Umoja wa Afrika Kanda ya Nne ngazi ya wataalamu, ambapo alisema kuwa dhamira ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira bora ya kukuza michezo nchini.
“Uwekezaji huu umetoa ujumbe mkubwa wa dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kukuza michezo kama ajira na chanzo cha mapato kwa vijana wetu,” alisema Msigwa.
Akizungumzia kuhusu mkutano huo alisema umejikita kujadili mikakati ya kikanda ya kuendeleza michezo na kuhakikisha vijana kutoka nchi 14 wanachama wa kanda hiyo wananufaika kwa njia ya maendeleo ya vipaji, ajira, na uchumi.
“Wataalamu wamewasilisha rasimu ya Mkakati wa Maendeleo ya Michezo ambao unaonyesha njia bora ya kusukuma mbele ajenda ya michezo, kuandaa mashindano ya vijana na kuwawezesha kushiriki kimataifa,” alisema Msigwa.
Aidha, alisema kupitia programu maalum, Kanda hiyo inalenga kutumia michezo kama kichocheo cha ukuaji wa uchumi kwa nchi wanachama huku ikiendeleza vipaji vya vijana.
Kwa upande wake Mkurungezi wa Maendeleo ya michezo ,Boniface Tamba alisema mkutano huo unafanyika kwa siku tatu huku ukiwa umegawanyika katika sehemu kuu nne awamu ya kwanza ni kikao cha wataalamu.
The post Msigwa: Uwekezaji kwenye michezo umelipa first appeared on SpotiLEO.