DAR ES SALAAM:SERIKALI imepokea msaada wa Sh milioni 30 kutoka Benki ya NMB kwa ajili ya kununua tiketi za mashabiki pamoja na motisha kwa wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), kuelekea mchezo wa robo fainali ya CHAN dhidi ya Morocco utakaochezwa Ijumaa hii, Agosti 22, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam leo wakati wa makabidhiano hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aliishukuru benki hiyo kwa mchango huo akisema ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza michezo nchini.
“Tunaishukuru Benki ya NMB kwa fedha walizozitoa kwa lengo la kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika michezo, kuhakikisha timu yetu ya taifa inafika hatua ya fainali katika mashindano haya ya CHAN,” Amesema.
Aliwaomba wadau wengine kujitokeza kuisaidia Taifa Stars, huku akiwataka Watanzania kujaza uwanja ili kuisapoti timu hiyo.
Kwa upande wake, Donatus Richard, mwakilishi wa NMB, alisema kati ya fedha hizo, Sh milioni 20 zitatumika kununua tiketi kwa mashabiki na Sh milioni 10 ni motisha kwa wachezaji.
Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, aliipongeza Taifa Stars kwa kufuzu robo fainali bila kupoteza mchezo wowote na kueleza imani yake kuwa kikosi hicho kitawapa Watanzania heshima kwa kuifunga Morocco.
“Huu ni mwaka wa kombe kurudi nyumbani. Tuna kikosi kizuri na tunawaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi. Kauli mbiu yetu ni ‘Hii Nimo’,” alisema Kamwe.
The post NMB yachangia milioni 30 kuiunga mkono Taifa Stars first appeared on SpotiLEO.