Na Mwandishi Wetu, Arusha
Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeanzisha mpango maalum wa kushirikiana na wanasheria ili kuimarisha usalama wa waandishi wa habari kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na historia ya matukio yanayojitokeza wakati wa chaguzi, ambapo waandishi wa habari mara nyingi hujikuta katika mazingira hatarishi kama vile kukamatwa, kutishiwa, kufunguliwa mashtaka au kuingiliwa katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ripoti ya Ukiukwaji wa Uhuru wa Vyombo vya Habari ya MCT ya mwaka 2022 ilionesha kupungua kwa matukio ya ukiukwaji kutoka 119 mwaka 2018/19 hadi 18 mwaka 2022. Hata hivyo, bado changamoto zinaendelea, ambapo matukio 27 yaliripotiwa mwaka 2024 na mengine 17 yameripotiwa kati ya Januari na Agosti 2025. Ukiukwaji huo unahusisha vitendo vya kukamatwa, vitisho, utekaji nyara, maonyo, kusimamishwa kazini pamoja na kuingiliwa kwa uhuru wa uhariri.
Huduma ya msaada wa kisheria kwa waandishi wa habari inatolewa kwa ufadhili wa International Media Support (IMS). Kupitia mpango huo, MCT inatoa mafunzo kwa mawakili watakaotoa msaada wa kisheria kwa waandishi wa habari katika mikoa ya Arusha, Mwanza na Zanzibar.
Rasmi, mafunzo hayo yamezinduliwa leo Agosti 19, 2025, jijini Arusha, ambapo mawakili 20 wa haki za binadamu wamepatiwa mafunzo ya siku moja. Mawakili hao tayari waliwahi kufundishwa na MCT katika vipindi vya mwaka 2021, 2022 na 2023. Mafunzo haya yameongozwa na Jaji Mstaafu Robert Makaramba, yakijikita kwenye sheria zinazohusu vyombo vya habari ikiwemo Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari na Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Aidha, wanasheria hao wamefundishwa mbinu za vitendo za namna ya kuwatetea waandishi wa habari watakaokumbana na changamoto za kisheria, hususan katika majukumu ya kuripoti uchaguzi na masuala yanayohusu jamii. Wamesema mafunzo hayo yamewaongezea uwezo wa kutetea haki za kikatiba na kusaidia kulinda misingi ya kidemokrasia nchini.
Kwa upande mwingine, MCT imeanzisha fursa maalum ya mazungumzo ya faragha kati ya waandishi wa habari na wanasheria kuhusu changamoto zinazowakabili. Huduma hiyo itatolewa jijini Arusha kwa siku mbili kuanzia kesho, Agosti 20, kabla ya kuhamia Mwanza na Zanzibar.
MCT inaamini kuwa jitihada hizo zitawawezesha waandishi wa habari kufanya kazi kwa kujiamini, kuripoti kwa weledi na bila hofu, huku wakifahamu kuwa kuna mtandao wa wanasheria wa haki za binadamu walioko tayari kuwasaidia kisheria wanapotekeleza majukumu yao