*Asema Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa wanapata haki na heshima wnayostahili
*Azindua Mpango kazi wa Kitaifa wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama
*Unalenga kushirikisha wanawake kikamilifu katika masuala ya Amani na Usalama
*Ataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutokomeza dalili zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani na usalama katika jamii
*Asema kuzinduliwa kwa mpango kazi wa Amani na Usalama kunaonesha jinsi Tanzania inavyoheshimu na kutekeleza makubaliano ya kimataifa
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Wanawake ni chanzo cha msukumo wa maendeleo katika Jamii hivyo Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa kila mwanamke nchini awe mama au mtoto wa kike anapata haki na heshima anayostahili.
Wakati Serikali ikiendelea kuhakikisha kuwa Wanawake nchini wanapata haki zao ikiwemo ya usalama na amani, ametoa wito kwao kuendelea kujitambua na kuchangamkia kila aina ya fursa inayojitokeza nchini.
Dkt. Biteko amesema hayo wakati akizindua Mpango kazi wa Kitaifa wa kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama 2025 – 2029 wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam ikiwa ni Azimio namba 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama.
Azimio hilo ambalo limeridhiwa na nchi zote Wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania linasisitiza na kutoa kipaumbele kwenye ushiriki kamili wa wanawake katika hatua zote za ujenzi wa amani, uzuiaji na utatuzi wa migogoro, mazungumzo ya amani, ulinzi wa amani na ujenzi mpya wa jamii baada ya migogoro.
.
Dkt. Biteko amesema kuwa kutekelezwa kwa Azimio hilo la Umoja wa Mataifa kunaonesha kuwa Tanzania si nchi inayoridhia tu mipango ya kimataifa inayowekwa bali inaheshimu makubaliano na maazimio ya kimataifa na hii inaifanya Tanzania chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan nikuzidi kuaminika Kimataifa na kuwa mfano wa kuigwa.
Akizungumzia, utekelezaji wa Ajenda hiyo ya Wanawake nchini Tanzania, Dkt. Biteko amesema kuwa “Tanzania tulishapiga hatua kubwa na tunaendelea vizuri katika kutekeleza Ajenda hii ya Wanawake, Amani na Usalama ambapo kwa mujibu wa Gender Inequality Index ya mwaka 2021, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilishika nafasi ya 146 kati ya nchi 191 kutokana na maendeleo yaliyopo tangu miaka ya 1990 katika kuhimiza usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake, kubiresha afya ya Mama na Mtoto pamoja na uwepo wa Uwakilishi wa Wanawake Bungeni.”
Ameongeza kuwa, mujibu wa Global Peace Index ya mwaka 2021; Tanzania ilishika nafasi ya 58 kati ya nchi 163 zilizo na hali bora ya amani Duniani.
Akieleza kuhusu mafanikio.mengine yaliyofilkiwa katika Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama nchini, Dkt. Biteko amesema Tanzania imeendelea kuwapa Wanawake fursa za juu na za Maamuzi ambapo hadi.kufikia Mei, 2023 Uwakilishi wa Wanawake katika mfumo wa Mahakama umefikia asilimia 46.6.
Ameongeza kuwa asilimia 22 ya Askari Polisi ni Wanawake na asilimia 30 ya Maafisa Uhamiaji ni Wanawake vile vile, Tanzania Bara ina Mawakili wa Serikali 785 ambapo kati yao wanawake ni 410 sawa na asilimia 52.
Ameeleza kuwa kwa upande wa Zanzibar, kuna jumla ya Mawakili wa Serikali 76 ambapo Wanawake ni 34 sawa na asilimia 44 ya Mawakili wote hivyo kwa hatuo hizo zilizopigwa na Tanzania nchi haina budi kujipongeza.
Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Biteko amesema kuwa bado kuna masuala ambayo yanahitaji kupewa msukumo ili kuleta haki na usalama kwa wanawake kwani takwimu zinaonesha kuwa asilimia 48.3 ya wanawake wote Tanzania wamewahi kufanyiwa ukatili wa aina mbalimbali, ambapo mwaka 2015 asilimia 65 ya wanawake waliogombea nafasi mbalimbali za uongozi walikutana na changamoto ikiwemo za matusi huku asilimia 17 ya wanawake hao wakishambuliwa na asilimia 13 wakiombwa rushwa ya ngono.
Amesisitiza kuwa takwimu hizo zinaonesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuinua haki ya mwanamke hivyo mpango huo uliozinduliwa unalenga kuhakikisha kuwa matendo yasiyo ya haki kwa wanawake yanatoweka na hadhi ya mwanamke inapanda kuliko sasa.
Aidha, Dkt. Biteko amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuutekeleza mpango huo wa amani na usalama kwa nguvu kubwa ikiwemo kutoa elimu na kutokomeza dalili zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani na usalama ikiwemo mila na desturi zinazoweza kuleta madhara kwenye jamii, wahamiaji haramu, unyanyasaji wa kijinsia na matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ametaja baadhi ya vipaumbele vya Mpango wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama kuwa ni uzuiaji wa migogoro, ushiriki wa wanawake katika kufanya maamuzi kwenye ngazi zote katika mikataba ya amani na kuwalinda wanawake na wasichana dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia wakati na baada ya migogoro .
Amesema.kuwa mpango huo utaleta matokeo chanya kwenye masuala ya amani na usalama kwa wanawake na kuwezesha Serikali kutimiza wajibu wake kitaifa, kikanda na kimataifa katika kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu kwenye masuala hayo ya amani na usalama.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Stergomena Tax amesema uzinduzi wa mpango huo ni tukio la historia na lenye uzito si kwa taifa tu bali kimataifa katika kujenga dunia yenye haki usawa na amani.
Ameongeza kuwa, ni kielelezo thabiti cha dhamira ya Serikali katika ushirikishaji wanawake katika masuala ya amani na usalama na uongozi.
Amemshukuru Rais Samia kwa kuwa sauti ya kimataifa katika kuhakikisha kuwa Dunia inakuwa na haki na amani na hii imepelekea Tanzania kutambulika duniani kwa kutoa mchango mkubwa katika misheni za kuleta amani ambapo hadi sasa Tanzania imeshatoa takriban askari 1500 katika misheni za kuleta amani na idadi hiyo ikijumuisha wanawake na wanaume.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto – Zanzibar, Mhe. Riziki Pembe ameeleza kuwa Mpango wa Ajjenda ya Wanawake, Amani na Usalama uliozinduliwa ni muhimu kwa maendeleo ya wanawake wote na Tanzania kwani maendeleo yanazidi kuchipua pale kunapokuwa na amani na usalama.
Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatekeleza ajenda hiyo kwa vitendo kwani nafasi za uongozi kwa wananwake zimeongezeka, mfano ukiwa ni uteuzi wa majaji wanawake wasiopungua sita ambapo hapo nyuma idadi ilikuwa chini ya hapo, pia Serikali inazingatia bajeti za masuala ya kijinsia kwa wizara zote .
Naye, Anna Mutavati, Mkurugenzi wa UN- Women katika Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, ameipongeza Tanzania kwa kuzindua ajenda hiyo ya Usalama na Amani kwa wanawake na kueleza kuwa inaendelea kuwa mfano wa kuigwa katika masuala ya amani na usalama ikiongozwa na Amiri Jeshi Mkuu amabye ni Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.