Hatimaye majuzi nimeambiwa Yanga imekubali kumuuza Mzize kwenda Esparance kwa dau la Dola 1 milioni ambalo msimamizi wake Jasmine alikuwa haamini mchezaji angeweza kuwa na thamani hiyo. Yanga wamepata walichokiamini, lakini hatujui kama msimamizi wa mchezaji amekipata alichokitaka.
Na sasa Mzize atakwenda zake Tunisia. Binafsi hakukuwa na ofa za kwenda naona ni dili nzuri kama hakukuwa na ofa za Ulaya. Huu ulikuwa wakati wake wa kwenda Ulaya moja kwa moja. Mbwana Samatta alitua Ulaya akiwa na miaka 23. Mwenyewe alikiri alichelewa kwenda Ulaya. Leo Mzize anaanza safari ya ndani ya Afrika huku pasipoti yake ikionyesha ana umri wa miaka 22
Wazungu wanalitazama kwa makini suala la umri kwa sababu mchezaji kwao ni biashara. Wanaangalia uwezekano wa mchezaji ambaye wataweza kumuuza ikihitajika kufanya hivyo. Kama hakukuwa na ofa kutoka Ulaya basi Mzize akazane ili walau afunge mabao mengi. Anaweza kupata dili la kwenda Ulaya ndani ya miaka miwili kwa sababu dunia ina uhaba wa washambuliaji kwa sasa.
Tukiachana na mambo ya kwenda Ulaya, hii ni hatua kubwa sana kwa Mzize. Anapaswa kutazamwa kama mfano wa kijana aliyeyapambania maisha yake. Kutoka kuendesha boda boda mtaani hadi kwenda kucheza moja kati ya klabu kubwa barani Afrika sio jambo la kawaida sana. Hakutoka katika akademi bora. Amejikuza mtaani mpaka ametimiza ndoto.
Kutoka kuendesha bodaboda hadi kuuzwa Dola 1 milioni ni kitu ambacho hata angewaambia wenzake wakati wakiwa katika maskani ya bodaboda, hakuna ambaye angeamini. Amebadili maisha yake katika namna ambayo inafanywa na wachezaji wengi wa Afrika Magharibi. Kitu kizuri zaidi kwa ninavyomuona anaonekana ni kijana mwenye nidhamu ndiyo maana kila siku kiwango chake kinapanda.
— Legend Edo Kumwembe.