Na Anangisye Mwateba-Katavi
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula amezitaka taasisi za Shirika la Hifadhi za Taifa na Bodi ya Utalii Tanzania kuwa na mpango wa pamoja kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi ya Taifa Katavi.
Mhe. Kitandula ameyasema hayo alipokuwa akiongea na uongozi wa Hifadhi ya Taifa Katavi Mpanda mkoani Katavi katika ziara ya kukagua uhifadhi na miundombinu ya utalii katika hifadhi hiyo.
Amesema Hifadhi hii ina vivutio vya kipekee ambavyo huwezi kuviona katika hifadhi nyingine mfano unaweza kuona kundi la nyati wengi wakitembea kwa pamoja kati ya 400 hadi 500 lakini pia kunz makundi makubwa ya ndege wanao hamahama hivyo vitu hivi vitangazwe ili kuvutia wageni wengi kuja katika hifadhi hii’
Katika ziara yake, Mhe. Kitandula alifika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi na kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Mhe. Lilian Charles Matinga akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrindoko.
Mhe. Matinga akitoa taarifa ya Mkoa wa Katavi ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kazi kubwa inayofanya katika kupambana na wanyama wakali na waharibifu husasani Tembo kupita taasisi za TAWA na TANAPA.
Aidha, Mhe. Matinga aliongeza kuwa asilimia 60 ya ardhi ya Mkoa wa Katavi imehifadhiwa kwa shughuli za uhifadhi wa wanyama na Misitu, hivyo shughuli nyingi za kiuchumi katika mkoa ziko chini ya Wizara ya maliasili na Utalii.
Naibu Kamishina wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa anayesimamia Kurugenzi ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Biashara, Missana Mwishawa amemshukuru Naibu Waziri kwa kutembelea Hifadhi ya Katavi kwa kuwa imewaongezea ari ya kufanya kazi kizalendo na kumuahidi kufanyia kazi yale yote aliyoyaelekeza kwa manufaa ya uhifadhi wa maliasili ili kuongeza idadi ya watalii pamoja na pato la taifa.
Hifadhi ya taifa ya Katavi imeanzishwa mwaka 1974 ambapo ni hifadhi ya tano kwa ukubwa ikitanguliwa na hifadhi ya Nyerere, Serengeti na Tarangire.