MARSEILLE: KLABU ya Olympic Marseille imewaweka sokoni Kiungo wake raia wa Ufaransa Adrien Rabiot na winga Mwingereza Jonathan Rowe kutokana na kile kilichotajwa na klabu hiyo kuwa “tabia isiyokubalika” kwenye chumba cha kubadilishia nguo baada ya kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligue 1 wiki iliyopita dhidi ya Stade Rennais.
Vyombo vya habari vya Ufaransa zilisema wachezaji hao wawili walizozana kwenye chumba cha kubadilishia nguo baada ya kufungwa 1-0 na Rennes, licha ya kuwa wenyeji wa mchezo huo ambao waliutawala kwa sehemu kubwa na kucheza na Rennes walio pungufu baada ya beki wao Abdelhamid Ait Boudlal kupata kadi nyekundu dakika ya 31.
Mzozo huo ulianza baada ya Rabiot kumshutumu Jonathan Rowe kwa kukosa ari ya kujitolea, shutuma zilizozua mabishano na wawili hao kurushiana matusi na kisha kuanza kupigana mbele ya wenzao, hadi pale wanausalama wa klabu hiyo walipolazimika kuingilia kati.
“Uamuzi huu umechukuliwa kutokana na tabia isiyokubalika ndani ya chumba cha kubadilishia nguo baada ya mechi dhidi ya Stade Rennais FC, kwa makubaliano na benchi la ufundi na kwa mujibu wa kanuni za ndani za klabu. Tayari wachezaji hao wamejulishwa juu ya uamuzi huu mapema Jumatatu” – imesema taarifa ya Marseille.
Rabiot na Rowe waliwasili Marseille mwaka jana na kuingia kikosini moja kwa moja huku wakiisaidia klabu hiyo kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligue 1 na kufuzu UEFA Champions League msimu huu.
The post Waliopigana ‘dressing room’ wapigwa bei first appeared on SpotiLEO.