PARIS: MENEJA wa mabingwa wa Ulaya Paris St Germain Luis Enrique anaamini mshambuliaji wake Ousmane Dembele anaweza kuwa imara zaidi msimu huu ukilinganisha na ule wa 2024/25, alipoisaidia klabu hiyo kutwaa ‘treble’ na kuibuka kuwa mmoja wa wawaniaji wakuu wa tuzo ya Ballon d’Or.
Dembele mwenye umri wa miaka 28 ni kama alitoka kwenye kivuli cha nyota wa zamani wa klabu hiyo Kylian Mbappe msimu uliopita na kuonekana kuwa muhimu katika ushindi wao wa Ligi ya Mabingwa na kuendelea kuvuma kwenye Kombe la Dunia la Klabu, ambapo PSG walimaliza washindi wa pili.
Dembele aliyefunga mabao 35 na kutoa pasi za mabao 16 msimu uliopita, alifufua matumaini ya PSG kwenye UEFA Super Cup wiki iliyopita, akimtengenezea Goncalo Ramos bao la kusawazisha dakika ya 94 kabla ya kipa wao mpya Lucas Chevalier kuzoa sifa kwa kuokoa michomo katika ushindi wao wa penalti dhidi ya Tottenham Hotspur.
“Nadhani msimu huu utakuwa na changamoto kubwa kwa Ousmane. Msimu jana alifanya maajabu, lakini nina hakika kwamba anaweza kuboresha aina yake ya uchezaji, bila shaka atakuwa mtu hatari zaidi msimu huu”.
“Lazima uwe jasiri sana kusema hivyo kuhusu Dembele, lakini nadhani tayari amekifikia kiwango hicho. Ni mchezaji muhimu sana kwetu. Ana sifa zaa ushambuliaji na pia anafranya vyema kutusaidia katika safu ya ulinzi. Naona alivyo na furaha natumai mwaka huu utakuwa bora zaidi.” – Luis Enrique aliwaambiia wanahabari kuelekea mechi ya leo Ijumaa dhidi ya Angers.
Mechi hii itakuwa ya kwanza kwa PSG katika uwanja wao wa nyumbani wa Parc des Princes ndani ya miezi mitatu ikiwa ni mechi ya kwanza ya nyumbani kwa kipa mpya Chevalier na beki Illia Zabarnyi. Klabu hiyo pia itawaonesha mashabiki mataji yao matano (Ligue 1, French Cup, Ligi ya Mabingwa, French Super Cup na UEFA Super Cup)
The post “Dembele atawaka sana msimu huu” – Enrique first appeared on SpotiLEO.