Achana na hiyo picha iliyoko mbele ya macho yako ambayo kuanzia jana ilivyopigwa mpaka leo imekuwa picha pendwa mtandaoni.
Hao ni Wakuu wa Idara za Habari na Mawasiliano wa timu pendwa za Yanga SC na Simba SC. Mmoja Ali Kamwe. Mwingine ni Ahmed Ally.
Leo usiku Taifa letu la Tanzania litakuwa na mchezo wa kutafuta nafasi ya kuingia Nusu Fainali ya Mashindano ya CHAN kwa mara ya kwanza. Mpinzani wetu ni Morocco ambao ni mabingwa mara mbili wa michuano hii.
Tunawaheshimu Morocco, lakini hatuwaogopi. Kimsingi Amiri Jeshi Mkuu wa nchi Dr. Samia Suluhu Hassan ameshatimiza wajibu wake kwa kutoa kiasi cha Sh. Mil 200 kwa wachezaji wa Stars kwa ajili ya kuongeza morali ya mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Makocha wameshazungumza jana katika Mkutano na Wanahabari. Kila mmoja ameshatimiza wajibu wake. Tuliobaki na madeni ni makundi mawili. Sisi mashabiki jukwaani na wachezaji ndani ya kiwanja.
Tumebaki sisi tu. Lakini zaidi ni sisi mashabiki ambao ni sehemu muhimu zaidi inayohitajika kujaa katika dimba la Benjamin Mkapa.
Wingi wetu jukwaani ndio unapeleka deni kwa wachezaji kupambana kiwanjani. Mashabiki ni nyenzo muhimu ya ushindi katika usiku wa leo.
Hivyo mashabiki wafahamu wazi wana umuhimu mkubwa wa kwenda kuyajaza majukwaa ya uwanja na kutengeneza hamasa kwa wachezaji wetu kiwanjani.
Mashabiki wana mchango mkubwa katika jioni ya leo. Hata benchi la ufundi la Taifa Stars mara kadhaa limekuwa likizungumzia jambo la mashabiki kuja katika mechi za Stars. Jioni ya leo mashabiki ni muhimu zaidi.
Kila mmoja akitimiza wajibu wake kama ambavyo Rais Samia ametimiza kwa wachezaji inawezekana kabisa kama Taifa tukaandika historia mpya ya soka letu tukiwa pamoja.
Mungu Ibariki Tanzania. Mungu Ibariki Taifa Stars. PAMOJA INAWEZEKANA.