Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameikabidhi Timu ya Taifa ya Soka (Taifa Stars) kiasi cha Shilingi Milioni 200 ikiwa ni sehemu ya hamasa na motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi kuelekea mchezo muhimu wa robo fainali dhidi ya Morocco utakaopigwa leo Agosti 22, 2025.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema fedha hizo ni zawadi ya Rais kwa mashujaa wa Taifa Stars ambao wameandika historia kwa kufuzu hatua hiyo ya robo fainali.
“Mheshimiwa Rais ameona ni vyema kuwatia moyo vijana wetu kwa kuwa hatua waliyofikia siyo ya kawaida. Hii ni ishara kwamba Watanzania wote wapo nyuma yao na wanawatakia ushindi katika mchezo dhidi ya Morocco,” alisema Prof. Kabudi.
Taifa Stars imekuwa ikionekana kama moja ya timu zilizoshangaza mashindano haya kwa kuonesha kiwango bora na kuondoa wapinzani waliokuwa wakipewa nafasi kubwa. Ushindi katika robo fainali utaipeleka timu hiyo moja kwa moja nusu fainali, hatua ambayo itakuwa historia mpya kwa soka la Tanzania.