DAR ES SALAAM: Rais wa Chama cha Golf cha Wanawake Tanzania (TWLG), Queen Siraki, leo amewaaga na kuwapa bendera ya taifa vijana wanne wa mchezo wa Gofu wanaotarajiwa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa nchini Mauritius.
Vijana hao Shufaa, Loyce, Ibrahim na Ramadhani wanatarajiwa kusafiri kesho, Agosti 24, na kurejea nchini Agosti 29 baada ya kushiriki katika mashindano yatakayowapa nafasi ya kupata uzoefu wa kimataifa, kukuza ujuzi wao, kuongeza kujiamini, na kujifunza zaidi kupitia ushindani wa kiwango cha juu.
Akizungumza wakati wa kuwaaga vijana hao, Siraki amewataka wakaitangaze vyema Tanzania kwa nidhamu, bidii na kuonyesha vipaji vyao uwanjani. Aidha, ameeleza kuwa safari hiyo ni hatua muhimu si tu kwa maendeleo ya wanamichezo hao binafsi, bali pia kwa ukuaji wa mchezo wa Golf hapa nchini.
“Najivunia kuona vijana wetu wanakwenda kupeperusha bendera ya taifa kupitia mchezo huu wa kiungwana. Ni matumaini yangu kuwa watarejea na uzoefu ambao utakuwa chachu kwa wachezaji wengine hapa nyumbani,” amesema.
Vijana hao pia wametajwa kuwa mabalozi wa mchezo wa Golf kutoka Tanzania, wakitarajiwa kuhamasisha na kushirikisha vijana wengine katika michezo kama njia ya kujijenga kijamii na kitaaluma.
The post Rais TWLG awaaga vijana wanne wanaokwenda kuiwakilisha TZ first appeared on SpotiLEO.