*Yaelezwa Sababu ni kupisha maandalizi ya Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu
Dodoma
Wizara ya Madini imetangaza kusogeza mbele Mkutano wa Saba (7) wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini uliokuwa ufanyike mwezi Novemba 2025 na badala yake mkutano huo utafanyika tarehe 19 hadi 21 Novemba 2026, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar EsSalaam.
Taarifa iliyotelewa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Eng. Yahya Samamba imeleza sababu za kusogezwa kwa mkutano huo kuwa ni kupisha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa nchini uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2025.
‘’Wizara ya Madini inaomba radhi kwa wadau wote wa ndani na nje ya nchi waliokuwa wanatarajia kushiriki Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini ambao ulipangwa kufanyika Novemba 2025,’’ imeeleza taarifa hiyo.
Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini nchini unaofanyika kila mwaka tangu 2019 ukibebwa na kaulimbiu mbalimbali, hutumika kama jukwaa la kujadili kwa pamoja mstakabali wa Sekta ya Madini, kubadilishana ujuzi, maarifa na uzoefu pamoja na kuangazia fursa mpya zinazojitokeza katika Sekta ya Madini nchini.
Vilevile, mkutano huo hutumika kuimarisha mazingiraya uwekezaji, kuendelea kuvutia uwekezaji mpya kutoka ndani na nje ya nchi, wadau kupata fursa ya kujifunza Sera, Sheria na mikakati mipya ya Serikali na kujadili kwa pamoja masuala ya kisheria na uchumi yanayohusiana na Sekta ya Madini.
Mbali na hayo, kupitia hafla ya Usiku wa Madini ambayo huambatana na mkutano huo, hutumika kutoa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri katika Sekta ya Madini kupitia vipengele mbalimbali ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wao kwa Sekta ya Madini nchini.
Aidha, mkutano huo huyakutanisha makundi mbalimbali wakiwemo mawaziri wa madini kutoka nchi nyingine za Afrika, watendaji wakuu wa kampuni kubwa za madini duniani waliowekeza nchini, watafiti, mabalozi wanao ziwakilisha nchi zao hapa chini na nje ya tanzania, mashirika ya kimataifa.
Makundi mengine ambayo hushiriki mkutano huo ni pamoja na wachimbaji, wafanyabiashara wa madini, taasisi za fedha, vyuo vikuu na vya kati, taasisi za umma, taasisi binafsi zinazojishughulisha na madini, viongozi mbalimbali kutoka wizara, taasisi za umma, mikoa na halmashauri ambazo shughuli za madini zinafanyika.