DAR ES SALAAM:UZINDUZI wa Wiki ya Simba utafanyika nje ya Dar es Salaam, ambapo mwaka huu shamrashamra zitaelekezwa Mafinga, Iringa, Agosti 31, 2025.
Mwaka jana ilikuwa Morogoro na mwaka huu klabu hiyo imesema imechagua Mafinga kutokana na wingi wa mashabiki na ukubwa wa tukio.
Msemaji wa Simba , Ahmed Ally, amesema Dar es Salaam Leo kuwa msafara wa magari aina ya Costa 10 utaondoka Dar es Salaam Agosti 30 kuelekea Mafinga. Magari hayo yatabeba viongozi wa Simba, waandishi wa habari na mashabiki zaidi ya 200, huku gharama za chakula na malazi zikibaki kwa washiriki wenyewe.
‘Simba na mashabiki wake wataanza shughuli kwa kufanya usafi Hospitali ya Wilaya ya Mafinga, kugawa zawadi kwa wagonjwa na kuweka miundombinu ya kusaidia wananchi. Baada ya hapo kutakuwa na maandamano makubwa mjini kuonesha mshikamano wa Wanasimba kabla ya uzinduzi rasmi kwenye viwanja vya Mafinga mjini,” amesema.
Amesema baada ya uzinduzi, matukio ya kijamii yatafuata kuanzia Septemba 2 ambapo Wanasimba kote nchini watashiriki siku ya kitaifa ya kuchangia damu. Ahmed alisema kila Mwanasimba ana jukumu la kuokoa maisha ya Watanzania na hata yeye atashiriki kutoa damu.
Septemba 3 kutakuwa na droo ya bonanza la matawi likihusisha timu kutoka Dar es Salaam na mikoani, mechi ya Simba Legends, pambano la wanawake na mchezo maalum wa vibonge. Septemba 4 itahusu uzinduzi wa matawi mapya ya Simba na Septemba 5 mashabiki watashiriki Biryani Day pamoja na watoto yatima.
Tarehe 8 Septemba, wachezaji, makocha na viongozi wote wa Simba watatoa msaada kwa kituo cha watoto yatima. Septemba 9 timu itafanya mazoezi na mkutano na waandishi wa habari kuelekea kilele cha Simba Day.
Simba Day yenyewe itafanyika Septemba 10, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo kutakuwa na burudani, utambulisho wa kikosi kipya na kutoa heshima kwa nyota waliotumikia klabu akiwemo nahodha Jonas Mkude anayestaafu baada ya miaka 15 na mshambuliaji John Bocco. Viingilio vimetajwa vitakuwa sh. 7,000 na sh. 350,000, huku tiketi za fainali ya Shirikisho dhidi ya RS Berkane zikibaki kuwa halali.
Kikosi cha Simba kinatarajiwa kurejea nchini Agosti 28, 2025 kikiwa kimetoka kambini Misri ambako kitapiga michezo miwili ya kirafiki kabla ya kuungana na mashabiki kusherehekea Simba Day.
The post Simba day kuzinduliwa Iringa Agosti 31 first appeared on SpotiLEO.