WOLVEHAMPTON: WACHEZAJI wa West Ham walikuwa na kazi ya ziada jana usiku baada ya kulazimika kumuondoa Nahodha wao Jarrod Bowen ambaye alikuwa tayari kuwakabili mashabiki waliokuwa wakizomea kufuatia kichapo chao cha 3-2 mbele ya Wolves katika mchezo Kombe la Carabao usiku wa kuamkia leo.
Bowen alionekana akimnyooshea kidole shabiki mmoja na kutoa lugha isiyofaa, kabla ya kuonekana kupandwa na jazba na kujaribu kuruka mbao za matangazo za kielektroniki na kuzuiwa na wachezaji wenzake
Kufuatia tukio hilo Bowen alitumia ukurasa wake wa Instagram kuomba msamaha kwa tabia hiyo mbele ya mashabiki wa West Ham waliosafiri umbali mrefu kuwaunga mkono katika dimba la ugenini la Molineux baada ya yeye na wachezaji wenzake kwenda kuwapongeza mwisho wa mchezo huo.
“Mimi ni mtu ambaye nina ‘passion’ na ninapambana kila wakati ninapoingia uwanjani najua nahitaji kuonesha mfano bora na ninyi mashabiki mnajua jinsi ninavyowapenda ninyi na klabu hii!” – Bowen aliandika.
The Hammers waliingia uwanjani wakiwa tayari wamepoteza michezo yao dhidi ya Sunderland na Chelsea kwenye Premier League, wakiruhusu mabao nane katika michezo hiyo na kumuacha meneja Graham Potter kwenye shinikizo kubwa wadau wengi wakitabiri atakuwa wa kwanza kufungashiwa virago msimu huu.
Katika mechi nyingine za mzunguko wa pili, klabu za Ligi Kuu ya England Leeds na Sunderland zilipoteza kwa mikwaju ya penalti dhidi ya wapinzani wa ligi ya chini Sheffield Wednesday na Huddersfield, huku Wrexham wakifunga bao la jioni na kuwalaza Preston 3-2.
The post Bowen aomba radhi mashabiki first appeared on SpotiLEO.