Na WMJJWM-Dar Es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imewahimiza wananchi kutumia huduma za msaada wa Kisaikolojia zinazotolewa na Maafisa Ustawi wa Jamii nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju, Agosti 27, 2025 wakati akifungua Mkutano wa Maafisa Ustawi wa Jamii katika Wiki ya Ustawi wa Jamii inayofanyika katika Viwanja vya Chuo cha Ustawi wa Jamii Kijitonyama Dar Es Salaam.
Wakili Mpanju amesema huduma za ustawi wa Jamii ni muhimu sana katika jamii hivyo amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii katika maeneo yao kwenye Halmashauri na Mikoa kutoa huduma hizo kwa wananchi kwa kuwafikia wananchi wenye changamoto mbalimbali za kiustawi na kuzitatua.
“Mkatoe elimu na huduma hizi kwa wananchi wenye huhitaji ili kusaidia kutatua changamoto mbalimbali, kwani changamoto za kiustawi zimekuwa zikisababisha matatizo katika familia na Jamii kwa ujumla.” amesema Wakili Mpanju
Aidha amewaagiza Maafisa Ustawi wa Halmashauri na Mikoa kushirikiana na wadau mbalimbali katika maeneo yao ili kusadiana katika kutatua changamoto mbalimbali za kiustawi katika jamii.
Amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua umuhimu wa uwepo wa kada ya Ustawi wa Jamii na mchango wake katika kuiletea jamii maendeleo. Hivyo inaendelea kuweka mazingira rafiki ya kuimarisha utoaji wa huduma hizo ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira za Maafisa Ustawi wa Jamii.
“Lakini pia Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi, kuweka mifumo ya kuratibu na kurahisisha ushiriki na wadau katika utekelezaji wa shughuli za ustawi wa Jamii.” ameongezea Wakili Mpanju
Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando amesema lengo la Mkutano huo wa Maafisa Ustawi wa Jamii ni kuwakutanusha Maafisa hao na kujadili namna ya kuboresha huduma za ustawi wa Jamii nchini ikiwemo mikakati ya kutatua changamoto zinazoikumba Kada hiyo na wananchi kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Rashid Mfaume amesema wataendelea kusimamia Afya zote za ustawi wa Jamii katika ngazi za Mikoa na Halmashauri kwa kuhakikisha kazi za Afisa Ustawi wa Jamii zinasimamiwa na Maafisa husika kwa ajili ya kutoa huduma sahihi za ustawi wa Jamii kwa wananchi wenye changamoto mbalimbali.
Mwenyekiti wa Maafisa Ustawi wa Jamii Martin Chuwa amesema Maafisa Ustawi wa Jamii wanahitajika katika jamii ili kutatua changamoto mbalimbali za jamii ambazo zinapelekea Jamii kukosa Ustawi hasa katika ngazi ya familia hivyo ameiomba Serikali kuendelea kuwaajiri Maafisa hao kwa wingi ili kukabiliana na changamoto hizo.
Naona baadhi ya Wadau wa maendeleo wamesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha huduma za Ustawi wa Jamii zinaboreshwa kuanzia ngazi za familia hadi taifa ili kuondokana na changamoto za kiustawi.