Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo (kushoto), akikabidhiwa Jarida la Hazina Yetu Toleo la Nne 2025, na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, Ofisini kwake Treasury Square, Jijini Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo (katikati), akiwa Katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha, baada akikabidhiwa Jarida la Hazina Yetu Toleo la Nne 2025, Ofisini kwake Treasury Square, Jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
…………
Na Josephine Majura WF, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, amekipongeza Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha Kwa kukamilisha Toleo la Nne la Jarida la Hazina Yetu linalozalishwa na Wizara kupitia Kitengo hicho.
Bi. Omolo ameyasema hayo Ofisini kwake Jijini Dodoma wakati wa kupokea Toleo la Nne la Jarida hilo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kutoka kwa Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha, Bw. Benny Mwaipaja, kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, ambalo huandaliwa na Kitengo hicho kila baada ya miezi mitatu.
Alisema kuwa Jarida hilo linamwonekano mzuri na makala pamoja na habari zake zimepangiliwa vizuri.
“Natoa rai kwamba muendelee kuhakikisha Jarida la “Hazina Yetu” linajikita kikamilifu katika kuonesha majukumu ya msingi ya Wizara ya Fedha ikiwemo usimamizi wa sera za fedha, ukusanyaji wa mapato ya Serikali, matumizi ya bajeti, na juhudi za kukuza uchumi wa Taifa” alisema Bi. Omolo
Alisisitiza kuwa Jarida hilo linapaswa kuendelea kuwa chombo cha kimkakati cha mawasiliano ya Serikali, kinachowasilisha kwa uwazi na kwa lugha rahisi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, pamoja na mipango ya muda mfupi na mrefu ya Wizara.
Aidha, alielekeza kuwa kila Toleo la Jarida liwe na muundo unaoakisi vipaumbele vya Serikali, likijumuisha makala maalum kuhusu miradi ya kimkakati, mafanikio ya kila robo mwaka, na changamoto zinazoshughulikiwa na Wizara.
“Ni muhimu sana kwa Kitengo chetu kuhakikisha taarifa hizi zinazotolewa zinawafikia wananchi wengi zaidi na kwa wakati kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano mlizonazo,” alisisitiza Bi. Omolo.
Akizungumzia mabadiliko ya kidijitali, Bi. Omolo alieleza kuwa wananchi wa sasa wanategemea kupata taarifa kupitia mitandao ya kijamii, tovuti rasmi za Serikali, na machapisho ya kidijitali, hivyo, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kiendelee kutumia mikakati madhubuti ya kufikia makundi mbalimbali ya jamii kwa kutumia majukwaa hayo kwa ufanisi.
Katika hatua nyingine, Bi. Omolo alitoa pongezi kwa Kitengo hicho kwa juhudi wanazozifanya katika kuhabarisha wananchi kuhusu majukumu na mafanikio ya Wizara ya Fedha na Serikali kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Bw. Benny Mwaipaja, aliahidi kuongeza juhudi na kuimarisha mbinu za mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu majukumu ya Wizara.
Bw. Mwaipaja alishukuru kwa pongezi zilizotolewa na Naibu Katibu Mkuu Bi. Jenifa Christian Omolo kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba kwa Kitengo cha Mawasiliano nankwa uwezeshaji wa kufanikisha majukumu ya Kitengo na kuahidi kuwa ushauri na maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu yatatekelezwa kikamilifu na kutumika kama mwongozo wa kuboresha zaidi Jarida la “Hazina Yetu” ili liendelee kukata kuu ya kihabari ya wadau wa Wizara.