Mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania (Twiga stars), Opah Clement ametambulishwa kama mshambuliaji mpya wa timu ya Wanawake ya SD Eibar inayoshiriki ligi kuu ya wanawake nchini Hispania kwa uhamisho huru akitokea Juarez Femenil ya Mexico.
Opah anakuwa Mtanzania wa kwanza kucheza Ligi Kuu ya Uhispania, huku akiwa Mtanzania wa pili kucheza katika ligi kubwa barani Ulaya nyuma ya Aisha Masaka anayechezea klabu ya Brighton ya ligi kuu ya England.
Nahodha huyo wa Twiga Stars mwenye umri wa miaka 24 amewahi kuvitumikia vilabu vya Simba Queens, Kayseri Kadin na Besiktas za uturuki na Henan Jianye ya China kwa nyakati tofauti.