DAR ES SALAAM: SIMBA imemtambulisha rasmi mchezaji wake mpya, Selemani Mwalimu akitokea Wydad Cansablanca ya Morocco.
Mchezaji huyo alitajwa kutua Simba kipindi hiki cha usajili kwa mkopo na hatimaye mambo yamekamilika yuko tayari kuwatumikia wekundu hao wa Msimbazi.
Safari yake ya soka ilianzia timu za vijana akiwa na Fountain Gate Academy (FGA Talents FC) katika Ligi ya Mabingwa ya Tanzania.
Mwaka 2023, alijiunga na Singida Black Stars kwa mkataba wa miaka mitatu na nusu na baadaye akapelekwa KVZ ya Zanzibar kwa mkopo msimu wa 2023-24 ambapo katika mechi 27 alizocheza alifunga mabao 20 huku akitoa pasi 7.
Kwa msimu wa 2024–25, alikwenda Fountain Gate ambapo aling’ara zaidi baada ya kufunga mabao manne katika mechi sit ana kuibuka mchezaji bora wa Septemba 2024.
Februari 2025, alijiunga na Wydad AC ya Morocco kwa mkataba wa miaka minne na nusu.
Simba imefanya usajili wa wachezaji wengi msimu huu kwa lengo la kuboresha kikosi chake na kurejea kwenye ligi wakiwa imara na kiushindani kuelekea kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania bara na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
The post Selemani Mwalimu mambo safi Simba first appeared on SpotiLEO.