MUNICH: MENEJA wa Bayern Munich Vincent Kompany amesema klabu za Bundesliga zinapata wakati mgumu kubakisha wachezaji wao bora kutokana na jeuri ya kifedha ya Klabu za Ligi kuu ya England ambazo zinanufaika na kiasi kikubwa cha mapato yatokanayo na uuzwaji wa haki za matangazo ya ligi hiyo kwenye TV.
Bundesliga imepoteza wachezaji bora walionaswa na klabu vya Premier League mwisho wa msimu uliopita, akiwemo Jeremie Frimpong, aliyejiunga na mchezaji mwenzake wa zamani wa Bayer Leverkusen Florian Wirtz Pamoja na Hugo Ekitike wa Frankfurt waliotua Liverpool, huku Benjamin Sesko, akihamia Manchester United.
Hata mchezaji aliyekuwa akiwindwa na Bayern Munich Nick Woltemademshambuliaji wa VfB Stuttgart kuna taarifa anaweza kutimkia EPL kunako klabu ya Newcastle United iliyoweka mezani ofa nono ya pauni milioni 63.
Kompany aliuambia mkutano na waandishi wa habari alipoulizwa ni nini kimesababisha hamahama hiyo ya wachezaji wa Bundesliga Kwenda EPL alijibu “Pesa”
“Nakumbuka nilipokuwa kocha wa Burnley kwenye Premier League, umekaa tu ghafla unajikuta una pesa za TV na ni milioni pauni milioni 100 kwa timu zilizopanda daraja. Kwa hiyo unatoka kwenye bajeti ya milioni 20-25 hadi milioni 120 au 130 ambazo kwenye Bundesliga ungeshindana na sita bora, nane bora,” alisema Kompany.
Klabu za Ujerumani zilizo kwenye madaraja mawili ya ligi zitagawana zaidi ya euro bilioni moja kwa mwaka chini ya mkataba mpya kwa miaka minne ijayo. Nchini England, Klabu za EPL pekee zinagawana zaidi ya mara tatu ya kiasi hicho kwa mwaka.
“Sunderland inanunua wachezaji, inawanunua kutoka Leverkusen tena inashindana na AC Milan. Huo ndio uhalisia wa misuli yao ya kifedha. Iko wazi wameweza kuendelea kwa miaka mingi, hasa kwa pesa za TV.” – aliongeza.
Kocha huyo amezishauri klabu za Bundesliga kutafuta njia mbadala za kuwabakisha wachezaji wao bora na kujilinda na kitisho cha pesa zinazotoka kwenye klabu za England. Amewataka pia viongozi wa ligi hiyo kuboresha maslahi ya kimikataba izisaidie kupata pesa zaidi zitakazoongeza ushindani wa ligi hiyo.
The post Kompany alia na ‘jeuri ya fedha’ ya EPL first appeared on SpotiLEO.