LONDON: WASHINDI wa Europa League Tottenham Hotspur wako mbioni kutangaza kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa RB Leipzig Xavi Simons kwa dau linalofikia euro million 60.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uholanzi tayari yuko nchini England, huku vyanzo mbalimbali vya Habari vikisema kuwa amekamilisha vipimo vyake vya afya kabla ya kusaini mkataba unaotajwa kuwa wa miaka mitano wa kuingia katika kikosi cha Thomas Frank.
Klabu hizo tayari zina makubaliano ya awali juu ya mchongo mzima ambao utamruhusu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 kuhamia Kaskazini mwa jiji la London, na maelezo kamili ya mchongo huo yakitarajiwa kukamilika ndani ya saa 24 zijazo.
Chelsea walifanya mazungumzo na Leipzig kuhusu kumnunua Simons mapema msimu huu lakini wanatazamiwa kukamilisha kwanza uhamisho wa pauni milioni 40 kumnunua Alejandro Garnacho wa Manchester United.
Simons sasa anatazamiwa kuungana na Joao Palhinha na Mohammed Kudus kama sajili mpya za Spurs msimu huu.
Spurs walishindwa katika jitihada zao za kunasa saini kiungo mshambuliaji wa Nottingham Forest Morgan Gibbs-White mapema msimu, huku mmoja wa wachezaji waliotajwa kumtaka sana Eberechi Eze akichagua kujiunga na wapinzani wao Arsenal kutoka Crystal Palace.
The post Simu ya Xavi Simons imepokelewa Spurs first appeared on SpotiLEO.