Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Morogoro
WAGOMBEA wa nafasi ya ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika mambo ya Mkoa wa Morogoro wamesema wananchi wa Mkoa wa huo watamchagua Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu kwa kuwa ametekeleza miradi mingi ya maendeleo ambayo ni kipaumbele cha wananchi.
Wakizungumza leo Agosti 29,2025 katika mkutano wa kampeni za Uraisi kupitia CCM Dkt Samia Suluhu Hasssn uliofanyika eneo la Tumbatu Mkoani Morogoro, mgombea ubunge Jimbo la Morogoro Mjini, Abdulaziz Abood, amesema katika manispaa hiyo upatikanaji nishati ya umeme umefikia asilimia 88.
Ameongeza kwamba shule za sekondari, msingi mpya zimejengwa huku sekta ya maji mradi mkubwa wa sh. bilioni 185 ambao wakati wowote utaanza kutekelezwa.
“Katika awamu hii kila unachoahidi kinatekelezeka, fedha za miradi zinakuja kwa wakati,” alisisitiza mgombea huyo wa ubunge.
Mgombea ubunge Jimbo la Mikumi, Dennis Londo, alisema mapinduzi makubwa yamefanyika katika mkoa huo ambao unakwenda kuwa kinara katika sekta za nishati, maji, usafirishaji na kilimo.
“Ujio wa SGR maelekezo yako kufungua barabara ya Mikumi – Kilosa sasa tunakwenda kubadilisha Wilaya ya Kilosa. Hakuna lugha ya kutumia zaidi ya kukupa kura za kishindo kwani kuna kata hazikuwahi kufikiwa na magari, umepeleka fedha Kata ya Kidunda ambako magari sasa yanapitika,” alisema.
Mgombea Ubunge Jimbo la Mvomero, Sara Msafiri alimpongeza Rais Dk. Samia kwa kutekeleza miradi ya maendeleo hususan miundombinu ikiwemo utekelezaji ujenzi wa reli ya SGR ambayo imerahisisha usafiri kwa wananchi wa mkoa huo na mikoa jirani.
“Tunaamini ukipata ridhaa, utakamilisha miradi yote ya kimkakati ya kitafa. Wilaya ya Mvomero ilikuwa na historia kubwa ya migogoro ya wakulima na wafugaji lakini ulipoingia madarakani, ulisema hali hiyo haiwezekani,” alieleza.
Alieleza kuwa kupitia programu ya Tutunzane, wakulima na wafugaji wamekuwa wakishirikiana katika shughuli mbalimbali za kijamii.
“Naomba nikuhakikishie kwamba, wananchi wa Mvomero na mkoa mzima wa Morogoro tutakupa kura za ndiyo mpaka kapu litamwagika,” alisisitiza.
Naye, mgombea ubunge Jimbo la Kilombero, Abubakar Asenga, wananchi wa Kilombero kwa sasa hawana changamoto ya barabara kuja mjini kwani wanatumia wastani a saa tatu badala ya saa sita.
Mgombea ubunge Jimbo la Ulanga, Salim Ashamu, alisema jimbo hilo limepata vituo vya afya vitatu, zahanati 21 kutoka tisa zilizokuwepo awali, vitongoji 70 vilikuwa na umeme mwaka 2020 lakini kwa sasa Zaidi ya vitongoji 170 vimefikishiwa huduma hiyo.
“Wananchi wanakwenda kukupa kura nyingi kwenda kuipeperusha bendera kwa miaka mingine mitano ili tushuhudie maendeleo makubwa zaidi. Tarehe 29 Oktoba tunakwenda kufanya kama vile ulivyotufanyia katika kipindi cha miaka mitano,” alibainisha.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mlimba, Jane – Rose Rwakatare, alieleza kuwa barabara zimejengwa, umeme umefika katika maeneo mengi vijijini, shule za kisasa zimejengwa hivyo hakuna wasiwasi katika uchaguzi wa Oktoba mwaka huu wananchi wanakwenda kuweka rekodi ya kumchagua Dkt Samia kwa kura nyingi za kishindo.