DAR ES SALAAM: JAMII ya Watanzania imeaswa kupenda sanaa za ndani ili kutunza utamaduni na maadili ya Kitanzania na kujiepusha na maudhui ya nje ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia katika kufifia kwa tamaduni, desturi lakini pia kuiinua sanaa ya Tanzania ambayo inakubalika pia nje ya nchi hususan katika nchi za Afrika Mashariki.
Wito huo umetolewa na Afisa Mwendeshaji Mkuu wa Azam Media Limited, Divisheni ya Maudhui na Utangazaji, Yahya Mohamed wakati akizungumza mbele ya wageni waalikwa kwenye usiku wa uzinduzi wa tamthilia mpya inayoitwa ‘Noma’ itakayoruka kila Wikiendi kupitia chaneli ya sinema zetu ya Azam TV.
“Sisi Azam Media tutaendelea kutoa nafasi kwa wabunifu mbalimbali wa kazi za sanaa, tunavyozungumza saa hizi tamthilia zetu zimeanza kuwa pendwa ukanda huu wa Afrika Mashariki, kupitia burudani hizi hata majirani zetu wameanza kukielewa Kiswahili na kutufuatilia”.
“Tunafahamu sanaa ni injini kubwa ya ajira za Watanzania lakini si hivyo tu, hii ni sauti ya Watanzania tuipende na tuipaze sauti yetu, tupeleke maudhui yetu yenye utamaduni na utambulisho wetu ili watu watuelewe kwakuwa sanaa ni daraja kubwa la kuelekea kwenye ulimwengu wa kimataifa. Sisi kama taasisi tutahakikisha tunaendelea kuwekeza kuhakikisha sinema zetu inaenda mbali zaidi” – Amesema Yahya Mohammed.
Kwa upande wake mzalishaji wa tamthilia hiyo Adam Kibaro amesema imebeba mambo tofauti na yaliyozoeleka kwenye macho ya Watanzania kikitumika kiwango kikubwa cha ubunifu na teknolojia na hadithi nzuri iliyobebwa na wasanii mahiri na wenye vipaji vikubwa.
Tamthilia hiyo kwa kiasi kikubwa imelenga kuipa jamii uelewa juu ya maisha ya wanaume wengi ambao wameyaficha mapito yao kwa tabasamu na kubadili msimamo wa wanaume waone kwamba kuelezea changamoto zao si dalili ya udhaifu.
“Tamthilia hii imeakisi kwa kiasi kikubwa maisha ya wanaume. Wanaume wanakutana bar, vijiweni, mitaani wanaongea na kucheka lakini nyuma ya kila mwanaume kuna jambo ambalo kutokana na jamii ilivyotuzoesha, inaonekana mwanaume kueleza changamoto zake ni udhaifu. Kwa hiyo tamthilia hii ikawaamshe wanaume na wana jamii wenye mtazamo huo” amesema Adam
‘Noma’ itaruka kila siku ya Ijumaa, Jumamosi na Jumapili kuanzia saa 1 usiku katika chaneli ya Sinema Zetu ndani ya Azam TV kuanzia Ijumaa ya Septemba 5, 2025.
The post “Watanzania tupende sanaa zetu” first appeared on SpotiLEO.