Mkurugenzi Mtendaji wa Manara TV, Haji Manara, amevunja ukimya kuhusu tetesi zilizokuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba huenda akarejea kufanya kazi katika klabu ya Simba SC.
Akizungumza kupitia kituo chake cha Manara TV, mwanahabari huyo maarufu alikanusha vikali taarifa hizo na kusisitiza kwamba hana mpango wa kurejea tena Msimbazi, kwani moyo wake upo kikamilifu ndani ya klabu ya Yanga SC.
“Nimeona na mimi nimetumiwa mitandaoni kwamba naenda kufanya kazi Simba, na watu wengi wamenipigia simu kuniuliza. Jibu langu ni hapana, sina mpango huo. Mimi naendelea kuwa mwanachama na shabiki wa Yanga, nalipa ada zangu na kufuatilia kila kinachoendelea ndani ya klabu yangu,” alisema Manara.
Haji Manara alikumbusha kuwa ni kweli aliwahi kufanya kazi ndani ya Simba SC, lakini kurudi huko hakumo kwenye ndoto zake. Aliongeza kuwa anaamini mitandao mara nyingine hutumika kwa makusudi kusambaza taarifa za uongo zenye lengo la kumchafua, hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Yanga SC unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ambapo yeye ni miongoni mwa wagombea wa nafasi ya Udiwani wa Kariakoo.
“Niwaombe wanachama na mashabiki wa Yanga wasipoteze muda kusikiliza hadithi za mitandaoni. Zipo zenye nia ovu, zenye malengo mabaya dhidi yangu. Moyo wangu uko Yanga na nitabaki kuwa Yanga daima,” alisisitiza.
Mbali na kufafanua msimamo wake wa mapenzi kwa Yanga SC, Manara pia aliwataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki kilele cha Wiki ya Yanga, akiwahimiza pia kununua jezi za timu yao. Alisema jezi hizo zina ubora wa hali ya juu na ni sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya klabu.
Kwa kauli hii, Manara ameweka wazi hatma yake ya soka na siasa, akibaki mshabiki na mwanachama wa Yanga SC huku akielekeza nguvu zake zaidi katika kugombea nafasi ya Udiwani Kariakoo kwenye uchaguzi ujao.