MANCHESTER: KLABU ya Manchester City imetangaza rasmi kumsajili kipa wa kimataifa wa Italia, Gianluigi Donnarumma kutoka Paris Saint-Germain kwa mkataba wa miaka mitano baada ya ‘kumpiga bei’ kipa wao Ederson kwenda Fenerbahce ya Uturuki.
Manchester City imelipa pauni milioni 30 kwa Donnarumma na ikakubali kumuuza Ederson kwa pauni milioni 12.
Mkurugenzi wa Soka wa City Hugo Viana amemwaga sifa kwa Donnarumma akisema rekodi za mshindi huyo wa UCL zinajieleza na ni furaha kubwa kuwa nae katika viunga vya Etihad.
“Amekusanya utajiri wa uzoefu wa hali ya juu na anajua kile kinachohitajika ili kufikia mafanikio katika kiwango endelevu.” amesema Viana
Kuondoka kwa Ederson kwenda Fenerbahce ya Uturuki kwa uhamisho wa kudumu, kulifungua njia kwa Donnarumma kusajiliwa City huku akitarajiwa kuingia moja kwa moja kikosini kuisaidia timu hiyo ambayo haioneshi dalili ya mwanzo mzuri wa ligi ikipoteza mechi mbili kati ya tatu ilizocheza.
Donnarumma mwenye umri wa miaka 26 alijiunga na PSG akitokea AC Milan mwaka 2021 na alikuwa kiungo muhimu katika ushindi wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa mapema mwaka huu pia kama sehemu ya kikosi kilichotwaa mataji matatu msimu uliopita kabla ya mambo kugeuka na kuonekana hatakiwi tena na Meneja Luis Enrique wa PSG
The post Donnarumma mmiliki mpya milingoti mitatu ya City first appeared on SpotiLEO.