DAR ES SALAAM: MSANII wa vichekesho nchini, Annastazia Exavery ‘Ebitoke’, ameibuka na ujumbe wa shukrani kwa mashabiki wake wote waliompa moyo, maombi na sapoti wakati alipokuwa akikabiliana na changamoto za afya ya akili.
Kupitia taarifa yake, Ebitoke amesema alijikuta akipitia kipindi kigumu kilichosababishwa na matatizo aliyodai yalihusiana na kulogwa, hali iliyompelekea kuathirika kisaikolojia.
“Ningependa kuchukua nafasi hii kuwashukuru kwa moyo mmoja mashabiki wangu wote na kila mmoja alieguswa na safari yangu. Upendo wenu mkubwa, maombi yenu ya dhati na sapoti yenu ya hali ya juu vimenitia moyo sana wakati nilipokuwa napitia changamoto ya afya ya akili,” alisema Ebitoke.
Aliongeza kuwa kila sala, ujumbe na maneno ya faraja aliyoyapokea kutoka kwa mashabiki wake yalimfanya ajisikie yupo karibu na familia kubwa yenye upendo wa kweli.
Kwa sasa msanii huyo amesema anaendelea vizuri kwa neema ya Mungu na ana matumaini mapya ya kurejea katika hali yake ya kawaida huku akiweka wazi kwamba nguvu alizonazo zimetiwa na upendo wa mashabiki wake.
Ebitoke ni miongoni mwa wasanii wa vichekesho waliopata umaarufu mkubwa kupitia mitandao ya kijamii na vipindi vya televisheni kutokana na ucheshi wake wa kipekee na utambulisho wake katika tasnia ya burudani.
The post Ebitoke awashukuru mashabiki kwa maombi first appeared on SpotiLEO.