TEXAS: MWANAMIELEKA Mark Calaway ‘The Undertaker’ amefunguka kwa mara ya kwanza kwa undani kuhusu safari yake ya kiroho, akieleza namna alivyorejeshwa kwenye imani ya Kikristo kupitia mke wake.
Katika ushuhuda wake, Undertaker alisema mwanzoni alisita kuhudhuria ibada kanisani kwa hofu kwamba “pengine nikipita mlangoni, Mungu atanichoma moto” kutokana na maisha yake ya nyuma na taswira aliyokuwa nayo. Hata hivyo, alikiri kuwa upendo na msukumo kutoka kwa mke wake ulimsaidia kurudia imani yake.
“Nilikuwa na hofu kubwa ya kuingia kanisani kwa sababu ya sura yangu – nywele ndefu, tattoo, na sifa niliyokuwa nayo. Lakini nilipoingia, nilihisi kupokelewa na kukubalika. Hapo ndipo niligundua upendo wa kweli wa Mungu kupitia mke wangu,” alisema Undertaker kwa hisia.
Akaongeza: “Ninamshukuru mke wangu kwa kuniangalia zaidi ya muonekano wangu wa nje. Kupitia yeye nimepata nafasi ya kuungana tena na Yesu Kristo. Nampenda sana.”
Undertaker alizaliwa Machi 24, 1965 huko Houston, Texas, Marekani. Alianza mieleka mwishoni mwa miaka ya 1980 na alijiunga na World Wrestling Federation (WWF), sasa WWE, mwaka 1990.
Kwa zaidi ya miaka 30, alitengeneza jina kubwa kwa kucheza mhusika wa kutisha mwenye heshima kubwa. Moja ya rekodi yake maarufu ni “The Streak”, ambapo alishinda michezo 21 mfululizo ya WrestleMania.
Alistaafu rasmi mwaka 2020 katika hafla ya Survivor Series, akihitimisha safari yake ya miongo mitatu katika WWE, na kubaki kama nguli wa mieleka duniani.
The post Mwanamieleka Undertaker aokoka first appeared on SpotiLEO.