BERLIN: Kiungo mshambuliaji wa Bayern Munich, Jamal Musiala amesema ana uhakika wa kurejea kwa kasi na ushindani katika msimu huu kwa mabingwa hao wa Ujerumani baada ya kuvunjika mguu na kifundo cha mguu katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu lililotamatika mwezi Julai.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 22 ni mchezaji muhimu kwa timu yake ya taifa kwenye mbio za kuelekea Kombe la Dunia 2026, alivunjika kifundo cha mguu baada ya kugongana na kipa wa PSG wakati huo Gianluigi Donnarumma katika mechi yao ya Kombe la Dunia la Klabu jijini Atlanta.
Katika mahojiano na jarida la SportBild Musiala alielezea hali yake akisema kwa sasa ameimarika pakubwa kwani anaweza kusimama na kutembea mwenyewe bila usaidizi wa mtu wala magongo ya kutembelea.
“Mguu unaendelea vizuri na unapona kama ilivyotazamiwa na madaktari, Sihitaji tena magongo naweza kutembea lakini sitaki kuharakisha mambo. Nitasubiri kwa muda unaohitajika”.
“Sitaki kuweka tarehe maalumu. Lakini kutokana na hatua niliyopiga hadi sasa nataka kucheza mechi za ushindani na Bayern mwaka huu. Kiakili wiki chache za kwanza hazikuwa rahisi kwangu. Lakini hakuna sababu ya kufadhaika kila mara kuhusu hali hiyo,” alisema.
Musiala, ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa na mabao 21 na asisti nane katika michuano yote Bayern ikitwaa ubingwa wa Bundesliga, hajamlaumu Donnarumma kwa kuumia kwake, akisema majeraha kama hayo ni kawaida katika soka.
The post Musiala aivutia kasi Bundesliga, ‘Champions League’ first appeared on SpotiLEO.