PARIS: BEKI wa Barcelona na timu ya taifa ya Ufaransa Jules Kounde ametoa wito wa kutathminiwa upya kwa kalenda ya soka inayozidi kuwa na msongamano na mrundikano wa mechi, akionya kuwa ratiba ya aina hiyo inaathiri si tu wachezaji pekee bali mfumo mpana wa mazingira katika soka.
Akizungumza kabla ya mechi ya kwanza ya Ufaransa ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Ukraine na Iceland, Kounde amesema wingi wa mechi hizo unaleta madhara si kwa wachezaji pekee bali ustawi wa familia zao pia.
“Sio tu wachezaji, Kuna familia. Pia nafikiria kuhusu watu wote wanaofanya kazi karibu na mfumo mzima wa soka na ambao wakati mwingine ni waathirika wa kasi hii ya mechi isiyo na kikomo.” – Kounde aliwaambia waandishi wa habari Jumatano.
Kounde, anayechezea Barcelona, hakucheza katika michuano iliyopanuliwa ya Kombe la Dunia la Klabu mapema mwaka huu, lakini mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 bado alidokeza athari za michuano hiyo kwenye msimu ambao tayari umejaa mechi.
Ufaransa itamenyana na Ukraine mjini Wroclaw, Poland, Ijumaa na Iceland jijini Paris Jumanne ijayo bila wachezaji Rayan Cherki wa Manchester City na William Saliba wa Arsenal ambao si sehemu ya kikosi cha mechi hizo kutokana na majeraha huku fowadi wa PSG Ousmane Dembele akikosa mazoezi ya Jumanne kutokana na jeraha la paja.
“Ni mfumo mzima wa ikolojia ya soka. Wakati mwingine katika maisha, tunapofanya mambo kupita kiasi, tunapoteza thamani yake. Tunapoona mambo mara kwa mara, hatuyapi tena umuhimu uleule. Hicho ndicho kinachotokea kwenye soka sasa hivi ni matumizi ya kupita kiasi ya wachezaji nadhani yanahitajika mabadiliko.” – aliongeza
Fainali za kwanza za Kombe la Dunia la Klabu ziliyoshirikisha timu 32 ziliongeza mechi 63 kwenye ratiba ya kawaida ya soka, huku PSGwaliofika fainali ya Kombe hilo, wakicheza mechi 65 katika msimu wa 2024-25. Jambo lililosababisha ukosoaji kutoka kwa wachezaji na klabu juu ya uchovu na hatari za majeraha.
Kounde alizitaka bodi zinazosimamia soka duniani kutafakari juu ya uendelevu wa wingi huu wa mechi na athari za muda mrefu kwenye soka.
The post “Utitiri wa mechi unaumiza wachezaji” – Kounde first appeared on SpotiLEO.