MALLORCA: KLABU ya Mallorca inayoshiriki ligi kuu ya Hispania LaLiga imemsimamisha na kumvua unahodha kiungo Dani Rodriguez baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 37 kulalamika hadharani kuhusu kuwekwa benchi kwenye mchezo waliopoteza dhidi ya Real Madrid wikendi iliyopita wakati familia yake ilikuwa uwanjani kumtazama.
Adhabu hiyo ilifuatia maneno ya Rodríguez kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo alilalamika kwamba watoto wake hawakuweza kumtazama akicheza kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Rodriguez, ambaye alijiunga na Mallorca mwaka wa 2018 na kuichezea zaidi ya mechi 250 za ligi alichapisha picha ya familia yake kwenye Instagram wakiwa kwenye uwanja huo, akionesha hasira yake ya kutocheza.
“Funzo muhimu na ushauri, Usitarajie chochote kutoka kwa yeyote, hasa nyakati hizi, ambazo heshima ya bidii ya kazi imekosekana, Usifanye jambo kwa kutarajia malipo. Fanya kwa ajili yako.”
“Inaumiza kuona mchezaji ambaye ndo’ amewasili, na kuhudhuria mazoezi mara moja tu, anapata fursa ya kucheza mbele ya wachezaji wenzake ambao wametumia miaka mingi kutetea jezi hii kwa jasho na kujitolea.” – Rodriguez aliandika.
Hasira za kiungo huyo zilionekana kuelekezwa kwa kocha Jagoba Arrasate ambaye alimpa mshambuliaji mpya Jan Virgili nafasi ya kucheza dakika ya 87 badala ya kiungo huyo.
Kufuatia chapisho hilo ndipo Klabu hiyo yenye makao makuu ndani ya Visiwa vya Balearic vya Hispania ikatoa taarifa ikisema Rodriguez “amesimamishwa kazi na kusitishiwa malipo,” na kwamba klabu “imemvua unahodha mara moja.”
Rodriguez hajazungumza lolote tangu klabu hiyo ilipomwadhibu
The post Kisa famila, nahodha Mallorca asimamishwa, avuliwa unahodha first appeared on SpotiLEO.