BERLIN: KOCHA wa Ujerumani, Julian Nagelsmann, ambaye mapema wiki hii aliweka lengo la kutwaa Kombe la Dunia la 2026, analazimika kurudi haraka kwenye michoro ya mpango wake huo kufuatia kipigo cha 2-0 kutoka kwa wenyeji Slovakia katika mechi yao ya kwanza ya kufuzu Kombe la Dunia la 2026.
Kikosi cha Nagelsmann, kilichojumuisha baadhi majina makubwa ya Ligi Kuu ya England kama Florian Wirtz na Nick Woltemade, hawakuwa na meno kabisa katika mashambulizi na makosa kwenye safu ya ulinzi huku wakionekana kukosa mpango wowote wa mchezo ambao Waslovakia waliwasambaratisha na kuwasababisha kichapo cha kwanza kabisa cha Ujerumani ugenini katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Wajerumani ambao pia walifungwa Ureno na Ufaransa katika ya UEFA Nations League mwezi Juni. Mechi yao inayofuata ya kufuzu Kombe la Dunia itakuwa nyumbani dhidi ya Ireland Kaskazini jijini Cologne Jumapili katika Kundi A, ambalo pia wamo Luxembourg.
“Mchezo haukuwa mzuri kwa kila mmoja wetu, Tuna nafasi ya kufanya mambo vizuri zaidi ndani ya siku tatu zijazo. Tumezungumza kuhusu Kombe la Dunia kabla ya mechi hii lakini lazima kwanza tufuzu. Kwa sababu kama tutacheza hivi kazi ya kufuzu itakuwa ngumu.” – alisema Kimmich
Mabingwa hao mara nne wa Dunia walitwaa Kombe hilo mara ya mwisho mwaka wa 2014 na tangu wakati huo wameshindwa kufurukuta kimataifa. Wakitolewa katika hatua ya makundi katika michuano miwili iliyopita ya Kombe la Dunia.
Nagelsmann, ambaye aliiongoza Ujerumani kutinga robo fainali katika ardhi ya nyumbani kwenye michuano ya Euro 2024, alisema Jumatano kwamba kuweka lengo la juu na kutaka kushinda Kombe la Dunia mwakani, ambalo litaandaliwa kwa pamoja na Marekani, Canada na Mexico, ni ishara kwamba timu hiyo iko katika hali nzuri.
Hata hivyo, baada ya kipigo kichungu cha Alhamisi, mashabiki wa Ujerumani wanataka timu yao ifanye haraka kurejesha makali yake na mabadiliko ya haraka, ikiwa ni pamoja na safu yao ya ulinzi iliyo hatarini huku beki wa kati Antonio Ruediger akionekana kupaliwa na mashambulizi yaliyozaa mabao yote mawili ya Slovakia.
Itakuwa muhimu kwa Nagelsmann kupata mchezaji muanzilishi, aliye tayari kuchukua jukumu la kutekeleza mpango wa wazi wa mchezo husika, huku Ujerumani ikionekana wazi kukosa muunganiko kati ya safu ya ulinzi na ushambuliaji.
The post Nagelsmann Presha inapanda, inashuka Ujerumani first appeared on SpotiLEO.