Kamanda Domina Mukama mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani.
Na Khadija Kalili, Michuzi TV
KAMANDA Domina Mukama mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani ametoa wito kwa Waandishi wa Habari kuzingatia weledi wao katika kuripoti habari za Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Akizungumza hivi karibuni kwenye mafunzo ya siku moja yaliyonyika Makao Makuu TAKUKURU Mkoa wa Pwani kamanda Mukama amesema kuwa wanahabari wote wanapaswa kuepuka kuandika habari ambazo ni za uchochezi na uvunjifu wa amani.
“Kuna madhara ya rushwa kisiasa, kiuchumi na kijamii kwani baadhi ya madhara ya rushwa kwenye uchaguzi nikama mpiga kura ama wapiga kura kukosa haki ya kumchagua kiongozi bora na anayemhitaji” amesema Kamanda Mukama.
Aidha Kamanda Mukama amesema kuwa “rushwa hukwamisha maendeleo kwani viongozi waliopatikana kwa rushwa wataishia kujilimbilizia mali na kutumia vibaya rasilimali za wananchi kurejesha fedha walizotumia”
“Waandishi mnapaswa kuelewa kuwa rushwa inadhalilisha utu wa wananchi kwa kuwafananishwa thamani zao na pombe,mavazi,khanga, fulana, vyakula na vitu vingine vidogovidogo wanavyopatiwa huku pindi wanapoingia madarakani jamii husika kutitimiziwa ahadi na kukosa huduma muhimu walizoahidi” amesema Mukama.
Wakili Leonard Swai Mkuu wa Dawati la Uchunguzi Mkoa wa Pwani amesema kuwa utafiti wa TAKUKURU kuhusu rushwa katika Umuchaguzi na uzoefu wake katika kazi amebaini kwamba katika kuelekea kipindi cha uchaguzi au wakati wa uchaguzi wagombea ama watia nia wamekua na mawakala wao pamoja na wao wakogawa magari ya wagonjwa, mifuko ya saruji, mipira ya miguu kuendesha harembee Makanisani na Misikitini,pia wamekua wakitoa michango mikubwa kwenye shughuli za kijamii ikiwamo misiba ,ugawaji wa pikipiki,baiskeli ambapo ugawaji huu hutafsiriwa kama rushwa na makatazo kwa maana ya sheria ya gharama za uchaguzi ambayo yanapaswa kuchunguzwa.
Aidha watoa mada wengine ni Anneth Mwakatobe Mkuu wa dawati la Elimu kwa Umma Mkoa wa Pwani ambaye amewasisitiza Waandishi wa Habari kuzingatia weledi na maadili ya kazi na kuzingatia suala la kutovaa nguo zenye viashiria ama rangi za Chama chochote cha siasa siku ya uchaguzi mkuu wa Rais ,Wabunge na Madiwani utakao fanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Wadau wengine ambao wamehudhuria kikao hicho ni viongozi wa dini zote na Mashirika yasiyo ya kiserikali NGO.