DAR ES SALAAM: Mwanamuziki mkongwe wa muziki wa Taarab, Khadija Kopa, amesema mashabiki ni nguzo muhimu kwa mafanikio ya msanii, lakini pia wanaweza kuwa chanzo cha kuanguka kwake kisanaa endapo hawatatumia vizuri nafasi yao ya ushawishi.
Kopa amesema kuwa mashabiki ndio wanaoamua hatma ya msanii wanaweza kumpa nguvu, au kumuangusha kabisa kwa kauli na matendo yao.
“Ili msanii akubalike, mashabiki wanapaswa kusikiliza kazi zake na kuzielewa. Wakizipenda, watampenda msanii, lakini msanii akikosea hata kidogo, haohao mashabiki wanaweza kumgeuka na kumuangusha,” amesema Kopa.
Kopa, ambaye pia ni mama mzazi wa msanii maarufu wa Bongo Fleva, Zuchu, aliongeza kuwa mashabiki wengi wamekuwa chanzo cha migogoro kati ya wasanii kutokana na tabia ya kuwapambanisha.
“Shabiki wa kweli hufurahia mafanikio ya msanii hata kama hayamnufaishi moja kwa moja. Tatizo linakuja pale mashabiki wanapoanza kuwasifia baadhi ya wasanii kwa kuwadhalilisha wengine, jambo linalochochea chuki isiyo ya lazima,” ameeleza.
Khadija ameitolea mfano mifarakano baina ya mashabiki wa lebo tofauti kama WCB na Konde Gang, akisema kuwa mara nyingi mivutano hiyo haianzi kwa wasanii bali kwa mashabiki wenyewe.
“Mfano mzuri ni pale shabiki wa WCB anapomchukia msanii wa Konde Gang si kwa sababu ya kazi zake, bali kwa matusi ya mashabiki wenzao. Au mtu kumchukia Nandy au Mimi Mars kwa sababu tu anampenda Zuchu. Hii siyo sahihi,” amesema Kopa.
Amesisitiza kuwa tabia hii inatengeneza uhasama wa kijinga na huathiri ukuaji wa muziki wa Tanzania kwa ujumla.
“Mabeef mengi yanatengenezwa na mashabiki. Badala ya kujenga, wanabomoa. Kwa nini tuwalinganishe wasanii? Kwa nini tusijenge wote wawe bora? Kiukweli, baadhi ya mashabiki wanaua vipaji vya wasanii wao bila wao kujua,” amemalizia.
The post Khadija Kopa: Mashabiki ndo kila kitu first appeared on SpotiLEO.