Kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Mwananchi, Klabu ya Yanga imetangaza kuwa siku ya Jumanne katika Makao Makuu yake yaliyopo Jangwani kutafanyika zoezi la uchangiaji damu salama kwa lengo la kusaidia watu wenye changamoto ya upungufu wa damu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, alisema shughuli hiyo itakuwa na umuhimu mkubwa kwa jamii kwani itagusa maisha ya watu wengi wanaohitaji damu hospitalini.
“Tutakuwa na mambo mawili. Moja ni kuchangia damu salama kuelekea Wiki ya Mwananchi kwa ajili ya kusaidia kundi kubwa la watu wenye changamoto ya ukosefu wa damu,” alisema Kamwe.
Aidha, alibainisha kuwa washiriki wote watakaojitokeza katika zoezi hilo maalum watazawadiwa zawadi mbalimbali kama sehemu ya kuonyesha kuthamini mchango wao.
Shughuli hiyo itahitimishwa kwa burudani ya pamoja ambapo washiriki na wageni wote watapata fursa ya kushiriki katika unywaji wa supu.